Mwalala twaenda kubandua Shandy kwao

MOMBASA. MATOKEO ya sare ya kutofungana ya mechi ya mkondo wa kwanza ya Caf Confederation Cup kati ya Bandari na Al Ahli Shandy ya Sudan sio mabaya kwa timu ya nyumbani ambayo inakwenda ugenini kutafuta ushindi ama sare ya kufungana.

Hayo yalikuwa maoni ya Kocha Mkuu wa Bandari FC, Bernard Mwalala ambaye anaamini matokeo hayo yanawapa moyo wa kwenda huko Sudan wakiwa na nafasi asilimia 50-50 ya kushinda pambano hilo na kuendelea mbele kwenye dimba hilo.

“Huenda baadhi ya wapenda soka wakafikiria ndio tumebanduliwa kutokana na matokeo hayo lakini kwetu hayo yanatupa moyo wa kuhakikisha tunapocheza mchezo wa marudiano, tutaanza kupigania bao la haraka tuwavunje nguvu wapinzani wetu,” akasema Mwalala.

Mkufunzi huyo alisema kuwa hawakucheza mchezo wao wa kawaida katika mechi hiyo ya Nairobi na watakapokuwako huko Sudan watachezaji mchezo wa kufunga na kuzuia wasifungwe hivyo waliwataka Wakenya wasiwe na wasiwasi.

Alisema furaha yake kubwa ni kuwa mechi hiyo ilimalizika ikiwa hakuna mchezaji yeyote aliyeumia ama kuonyeshwa kadi. “Hilo linanipa matumaini makubwa ya vijana wangu kucheza vizuri zaidi katika mchezo wetu wa marudiano na kuibuka washindi,” akasema.

Alisema safu yake ya kiungo haikufanya kazi yake vizuri na ndio maana washambulizi wake hawakupata mipira ambayo ingewawezesha kufunga mabao.

 “Tatizo hilo tutalirekebisha wakati huu tunajiandaa kwa mechi ya marudiano,” akasema.

Sababu nyingine aliyotoa Mwalala kwa kutopata ushindi kwenye mechi hiyo ni kuwa walikuwa hawajui wachezaji wa wapinzani wala jinsi wanavyocheza lakini sasa amewatambua, watarekebisha makosa na kupigania ushindi.