Nyota Simba, Yanga watangaza vita mpya CAF

Muktasari:

Simba na Yanga zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam ambayo ndio pekee iliyopoteza kwa bao 1-0 ugenini mbele ya Fesil Kanema ya Ethiopia na KMC ziko kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Dar es Salaam. HAKUNA namna hapa zaidi ya kupambana na wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa hakuna aliye salama mpaka sasa.
Simba, Yanga, Azam na KMC zote zinajipanga kwa mechi za marudiano ambazo ni lazima zishinde ili kusonga mbele hatua inayofuata. Simba na KMC zitakuwa nyumbani baada ya kulazimisha sare zikiwa ugenini huku Yanga ambayo nayo ilipata sare ya bao 1-1 dhidi Township Rollers ikisafiri hadi Botswana.
Simba na Yanga zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam ambayo ndio pekee iliyopoteza kwa bao 1-0 ugenini mbele ya Fesil Kanema ya Ethiopia na KMC ziko kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, matokeo hayo hayaonekani kuwakatisha tamaa baadhi ya wachezaji wa timu hizo na wamefichua kuwa vita ndio kwanza imeanza.
Beki mpya wa Simba, Gadiel Michael alisema kuna mambo wameyasoma kwa wapinzani wao, UD Songo ya Msumbiji na mchezo ujao pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ushindi ni lazima.
“Mchezo ni dakika 90, lakini kuna mambo yalikwamisha ushindi ugenini ikiwemo uwanja mbovu ila tunajipanga kumaliza kazi ili kufuzu hatua inayoafuata.
“Hakuna anayetamani kuona anawaangusha mashabiki wanaokuja kutuunga mkono, tuna matarajio makubwa na ninaamini ushindi upo tena wa mabao ya kutosha tu,” alisema.
Naye Haruna Shamte alipigilia msumari akisema suala la ushindi kwenye mchezo huo halina mjadala.
Shamte ni miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba msimu huu akitokea Lipuli ya Iringa.
Wakati mastaa wa Simba, wakionyesha matumaini ya ushindi kwenye mechi ya marudiano, Yanga hawapo nyuma licha ya kuwa watasafiri kwenda ugenini kwa Towship Rollers.
Kiungo wa Yanga, Fei Toto alisema soka halina kanuni za ushindi na suala la kuwa nyumbani ama ugenini sio ishu kwani, lolote linaweza kutokea.
“Kushinda kwa Rollers sio suala gumu, wanafungika vizuri tu na kikubwa ni kuweka dhamira ya kufanya kitu cha maana,” alisema.
Naye straika wa KMC, Salum Aiyee hakuwa nyuma akisema wana uhakika wa kushinda kwenye mchezo wa marudiano ambao utapigwa nyumbani.
“Kama tumepata sare kwao kwanini tushindwe kushinda nyumbani. Nina imani kubwa tutasonga mbele,” alisema.
Naye staa wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma alisema Yanga na Azam FC watatakiwa kuwa na kazi ya ziada kwenye mechi zao za marudiano, akidai matokeo yao yana mtego.
“ Rollers ilipata nafasi moja na ikaitumia, nafikiria kwao watakuwa vipi. Hapa lazima Yanga waende na tahadhari kuwa ili kupatra matokeo mazuri ugenini,” alisema.