Mbelgiji Simba aja na mbinu za kuiua Azam mapema

Tuesday August 13 2019

Mbelgiji Simba, tanzania aja na mbinu, za kuiua Azam, mapema, Mwanaspoti, Michezo, Mwanasport

 

By OLIPA ASSA

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba imeanza maandalizi yake ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba inafanya mazoezi yake kwenye viwanja vya Gymkhana chini ya kocha Patrick Aussems kwa lengo la kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kutetea taji hilo walililotwaa msimu uliopita kwa kuifunga Mtibwa Sugar jijini Mwanza.

Katika mazoezi hayo kocha aliwapanga wachezaji katika makundi tofauti akawaweka wawili wawili beki na mshambuliaji kufanya zoezi la kukaba na kushambulia.

Mwanaspoti online linakuletea namna ambavyo walikuwa wanashambuliana mastraika na washambuliaji, mabeki na viungo ambapo iliwachukua kama dakika moja kila mmoja.

Bocco vs Tshaballa

John Bocco alikabidhiwa kwa Mohamed Hussein 'Tshabalala' ndani ya dakika moja walitoana jasho, huku langoni akiwa amekaa Beno Kakolanya.

Advertisement

Bocco alionekana kutumia akili nyingi kumpita Tshabalala, ambaye alionekana kukamia ili mradi kumshawishi kocha Aussems kuendelea kumpanga kwenye kikosi cha kwanza.

Kagere vs Gadiel

Kazi ilikuwa kwa Meddie Kagere na Gadiel Michael beki mpya wa Simba ambao walikuwa wanapambana kama vile wanacheza mechi na timu pinzani.

Gadiel alijikuta akifanya kazi kubwa ya kupunguza kasi ya Kagere ambaye muda wote alionekana ana hamu ya kucheka na nyavu.

Hata hivyo Gadiel amewahi kuliambia Mwanaspoti kwamba alikuwa ana hamu ya kumjua Kagere kwa ukaribu kitu kinachokuwa kinampa nguvu ya kusumbua mabeki uwanjani.

"Kagere si mtu wa mchezo kwenye mazoezi, hana masiraha naona hilo ndilo jambo linalomfanya awe moto uwanjani,nimefanya naye mazoezi kwa hiyo nimemjua kwa sehemu,"anasema.

 Flaga vs Kapombe

Kapombe alionyesha umahiri wake kwa Mbrazil Flaga ambaye alimbana kisawasawa ingawa naye hakutaka kuonekana mzembe mbele ya kocha wao Aussems.

Gerson v Shamte

Shamte naye alionekana kupambania namba baada ya kumbana kisawa sawa Gerson ambaye alionekana analitamani gori ambapo alijikuta mipira inaishia mguuni kwa beki wake.

Mkude vs Wawa

Shuguli ilikuwepo kwa kiungo mkabaji na Pascal Wawa beki wa kati mabao walionekana kutoshana nguvu, hivyo hakuna ambaye alikubali kushusha thamani yake.

Ndemla vs Chama

Chama walikuwa wanapimana uwezo na Said Ndemla ambao walionekana kutumia akili zaidi kuliko nguvu.

Baada ya zoezi hilo walijinyosha viungo kisha wakaanza kuchezea mipira.

Advertisement