Geay: Wanariadha wa Tanzania tunakwenda Morocco kupambana

Muktasari:

Tanzania inashiriki mara ya 12 michezo ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne, ilianza kushiriki mwaka 1965.

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Tanzania katika Michezo ya Afrika (All Africa Game), Gabriel Geay amesema idadi ndogo ya wanamichezo wa Tanzania hakuwezi kuwafanya kuwa wanyonge.

Timu ya judo na riadha itaiwakilisha nchi kwenye michezo hiyo itakayofunguliwa Agosti 19 mjini Rabat, Morocco.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa bendera ya Taifa, mwanariadha huyo Geay alisema Tanzania haiwezi kuwa wanyonge kwenye michezo hiyo.

"Ni kweli tunakwenda idadi ndogo ya wachezaji, lakini hicho hakiwezi kuwa kikwazo, tutapambana kwa uchache wetu kuhakikisha tunafanya vizuri," alisema Geay.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini, Yusuph Singo aliyekabidhi bendera timu hiyo kwa niaba ya Waziri wa Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliwataka wanamichezo hao kushindana kikamilifu bila kujali idadi yao kwenye michezo hiyo.

Alisema hatarajii visingizio kwenye michezo hiyo mikubwa ambayo inashirikisha wanamichezo kutoka mataifa 54 ya Afrika.

"Naamini kila mmoja ana malengo ya kufanya vizuri na bahati nzuri wengi wenu ni wazoefu wa kimataifa, hivyo hamtotuangusha," alisema Singo.

Msafara wa kwanza wa Tanzania utaondoka nchini kesho Jumatano ambao utakuwa na wachezaji wa judo na viongozi, wakati wanariadha wakitarajiwa kuondoka Agosti 20.