Anthony Joshua, Andy Ruiz kumalizana Saudia

Saturday August 10 2019

 

By LONDON, ENGLAND

UBISHI lazima umalizwe. Ndio, lile pambano la marudiano kati ya Anthony Joshua na Andy Ruiz Jr limepangwa kufanyika Desemba 7 mjini Diriyah, Saudi Arabia.
Taarifa kutoka duru za masumbwi zimethibitisha kuwepo kwa pambano hilo la kuwania mataji ya IBF, WBA na WBO litafanyika Umangani, ikiwa ni siku mbili tu kabla ya Watanzania kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru.
Awali, Jiji la New York, Marekani na Uwanja wa Cardiff walikuwa wakiwania kuwa wenyeji wa pambano hilo, lakini wakazidiwa kete na Diriyah kufuatia Mamlaka ya Michezo ya Saudi Arabia kuweka kiasi cha Dola za Kimarekani 100 Milioni kupewa uenyeji huo na sasa itakuwa kazi tu ya mashabiki wa ngumi kujiweka mkao wa kushuhudia ndonga zikilika.
Juni mwaka huu Ruiz alimtwanga AJ na kubeba mataji hayo na Joshua kuomba kurudiana na mpinzani wake huyo aliyewashangaza mashabiki wa ngumi katika pambano hilo lilichezwa kwenye Ukumbi wa Madison Square Garden , New York Marekani.
Joshua ambaye amepigiwa upatu kumrithi bingwa wa zamani katika uzani huo Mohamed Ali aliangushwa mara nne kabla ya refa kuingilia kati na kusitisha pigano hilo kunako raundi ya saba.

Advertisement