Madrid waja kivingine kumnasa staa Neymar

MABOSI wa Real Madrid wameripotiwa kuwa wapo Paris kwenda kufanya mazungumzo na wenzao wa PSG kwa ajili ya kumnasa supastaa Neymar kwa dili la thamani ya Pauni 250 milioni.
Kwenye mpango huo, ripoti zinadai kwamba winga wa kimataifa wa Wales, mwanasoka aliyewahi kuvunja rekodi ya dunia ya uhamisho mwaka 2013, Gareth Bale atahusika kwenye dili hilo.
Kwa muda mrefu tangu mwishoni mwa msimu uliopita, Neymar amekuwa akielezwa kutaka kuachana na PSG huku kurejea Barcelona likitajwa kuwa ni chaguo la kwanza. Lakini, sasa uhusiano wa mabosi wa PSG na Barcelona umetibuka na kutubua kila kitu kuhusu mpango wa Mbrazili huyo kurudi zake Nou Camp kuungana na maswahiba wake, Lionel Messi na Luis Suarez.
PSG walitaka Barcelona wawape wachezaji pamoja na pesa ili wamchukue Neymar, lakini kwa namna mabingwa hao wa La Liga walivyomthaminisha mchezaji huyo limewachukiza wenzao na kutibua biashara nzima. Na baada ya makamu wa rais wa Barcelona kusema kwamba dili la Neymar limekufa, Real Madrid wakaingia haraka haraka kunasa saini yake.
Mwanzoni Los Blancos waliripotiwa kuweka mezani Pauni 110 milioni pamoja na kiungo Luka Modric, lakini sasa wameamua kumjumuisha Bale kwenye dili hilo la kuhakikisha Neymar anatua Bernabeu.
MISHAHARA MIKUBWA YA MASTAA ULAYA KWA WIKI
-Lionel Messi (Pani 900,000)
-Cristiano Ronaldo (Pauni 850,000)
-Antoine Griezmann (Pauni 725,000)
-Neymar (Pauni 675,000)
-Luis Suarez (Pauni 625,000)
-Gareth Bale (Pauni 600,000)
-Alexis Sanchez (Pauni 505,000)
-Philippe Coutinho (Pauni 500,000)