Bandari Kenya kuchafua hewa ya Shandy, Afrika

Thursday August 8 2019

Bandari Kenya, kuchafua hewa, ya Shandy, Afrika, Mwanasport, Mwanaspoti, Tanzania

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF

MOMBASA. NAIBU Kocha wa Bandari FC, Ibrahim Shikanda anaamini timu yake mpya inaweza kushinda pambano lake la kwanza la Caf Confederation Cup dhidi ya Al Ahli Shandy FC litakalofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Moi wa Kasarani jijini Nairobi Jumamosi.
Shikanda ambaye amesajiliwa na Bandari siku chache zilizopita amewakuta wachezaji wakiwa katika hali nzuri na tayari kwa mchuano huo ambao anatarajia timu yake hiyo kupata ushindi.
“Ni wiki moja pekee tangu nisajiliwe na kuanza kazi yangu mpya Bandari FC na ninachoshuhudia ni wachezaji kuwa na hamu na moyo wa kuwashinda Wasudan hao na kuweka tamaa ya kufanya vizuri hata ugenini,” alisema.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kusajiliwa kwake akiwa Uwanja wa Mbaraki Sports Club wakati wa kipindi cha mazoezi, Shikanda alisema tamaa yake kubwa ni kuwa wanasoka wao hivi sasa wana uzoefu wa kucheza mechi kubwa za kimataifa dhidi ya timu yoyote barani Afrika.
“Wakati wa ziara ya timu yetu hii huko Afrika Kusini na ushiriki wao wa Kombe la Cecafa Kagame, wachezaji wameweza kuonyesha viwango vya juu na hivyo nina imani kubwa watawika hapo Jumamosi,” alisema mkufunzi huyo.
Akitoa mafunzo kwa wachezaji wa timu hiyo pamoja na Kocha Mkuu, Bernard Mwalala na Naibu Kocha, Nassoro Mwakoba, Shikanda alipongeza umoja ulioko kati ya wanasoka, maofisa wa benchi la ufundi na viongozi wa klabu akisema umoja huo utazidi kuzalisha matunda kwenye timu.
“Nina furaha tele kwa uongozi wa Bandari kwa kunipa fursa ya kuwa miongoni mwa wakufunzi katika timu hiyo na ninaahidi nitafanya bidii zangu zote kuhakikisha tunafanikiwa kufanya vizuri kwa mashindano ya kimataifa na kitaifa,” alisema.
Kati ya timu ambazo Shikanda amewahi kuzitumikia ni pamoja na Tusker FC na Azam FC ya Tanzania.

Advertisement