Kocha Oktay acheza kama Kerr hapo Gor Mahia

Muktasari:

Oktay kajiuzulu baada ya kuwaongoza Gor kutwaa taji lao la 18 la Ligi Kuu pamoja na kuwafikisha kwenye robo fainali ya dimba la CAF Confederation na ndio itakayobakia historia yake kubwa kwani haijawahi kutokea.

Nairobi. Unaambiwa pale Gor Mahia, aliyekuwa kocha wao Mualgeria Hassan Oktay  kacheza kama mtangulizi wake Mwingereza Dylan Kerr.
Ishu ipo hivi. Baada ya kuomba siku kadhaa asafiri kwenda kwao kutokana na jambo la dharura, Oktay alifika nyumbani salama na baada ya siku kadhaa akawaandikia mabosi wa Gor barua ya kujiuzulu wadhifa wake.
“Tafadhali naomba mnikubalie nijiuzulu wadhifa wangu kama kocha wa Gor Mahia. Uamuzi huu umelazimishwa na changamoto za kibinafsi ninazopitia hapa Ulaya,” Oktay alimwandikia mwenyekiti wa klabu hiyo, Ambrose Rachier.
Ikumbukwe, ni kwa staili hiyohiyo ndiyo aliyoitumia Kerr kuwatoka Gor baada ya kusafiri kweda kwao Ulaya kwa ajili ya likizo fupi ili kuweka mambo yake fulani ya kibinafasi sawa.
Siku chache baadaye Gor walisafiri kwenda kushiriki mechi ya Sportpesa wakicheza dhidi ya Everton walikolimwa magoli 4-0. Kocha Kerr alisimamia mchuano huo. Baada ya mechi kumalizika, alitarajiwa angerejea na timu lakini siku chache baadaye akajiuzulu na ndipo Gor ikaibukia kwake Oktay ikimpa kazi Disemba mwaka jana na sasa naye kawatoka kwa staili hiyo.
Oktay kajiuzulu baada ya kuwaongoza Gor kutwaa taji lao la 18 la Ligi Kuu pamoja na kuwafikisha kwenye robo fainali ya dimba la CAF Confederation na ndio itakayobakia historia yake kubwa kwani haijawahi kutokea.
Chanzo cha kuondoka kwa kocha huyo bado hakijabainika ila vyanzo vinaarifu kuwa suala la kucheleweshewa mshahara, kunyimwa uwezo wa kufanya maamuzi ya usajili wa wachezaji pamoja na kupata ofa kadhaa ndizo zilizomtoa Oktay pale.
Oktay aliondoka mapema wiki iliyopita kipindi timu yake ikiwa inajiandaa kuanza msimu kwa kuvaana na mabingwa wa ligi ya Burundi, Aigle Noir ugenini kwenye michuano ya mchujo raundi ya kwanza kufuzu kushiriki dimba CAF Champions League msimu huu.