Kibadeni: Kanda wa Simba amtoa mafichoni Okwi

Muktasari:

Mchezaji huyo raia wa DR Congo ana vitu vyote vya msingi uwanjani kama Okwi, lakini anapaswa kuthibitisha Simba haikufanya kosa kumsajili.

Dar es Salaam. Kiwango cha winga mpya wa Simba, Deo Kanda alichoonyesha katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kimemuibua Kocha Abdallah Kibadeni.
Akizungumza jana, Kibadeni alisema Kanda anapita katika njia aliyopita aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Emmanuel Okwi.
Okwi alimaliza mkataba Simba na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara walinasa saini ya Kanda kuziba pengo lake.
Kibadeni alisema winga huyo anapaswa kuthibitisha ubora huo  ingawa katika mchezo wa juzi Jumanne alionekana kupita njia za Okwi.
“Okwi alikuwa akiamua matokeo ya Simba na Kanda anapaswa kuthibitisha hilo. Ameanza vizuri na ana uwezo mkubwa kisoka, kazi kubwa iliyobaki ni kuthibitisha kuwa viatu vya Okwi Simba vitamtosha,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba na Taifa Stars.
Alisema mchezaji huyo raia wa DR Congo ana vitu vyote vya msingi uwanjani kama Okwi, lakini anapaswa kuthibitisha Simba haikufanya kosa kumsajili.
 Kibadeni alisema mashabiki wa Simba bado wanamuota Okwi kwa  kuwa alikuwa mshambuliaji hodari mwenye kiwango cha kufunga mabao aliyeipa mafanikio klabu hiyo katika michuano mbalimbali.