Hazard afungua akaunti ya mabao Real Madrid, Bale mambo bado

Muktasari:

Hazard alicheza dakika 62, lakini winga Gareth Bale hakucheza mchezo huo ikiwa ni muendelezo wa uhusiano wake mbaya na Kocha Zinedine Zidane.

Madrid, Hispania. Mshambuliaji Eden Hazard amepiga bao la kwanza Real Madrid usiku jana katika mechi walioshinda bao 1-0 dhidi ya Red Bull Salzburg.

Hazard alifunga bao maridadi katika mechi hiyo ya maandalizi ya msimu mpya ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipotua Santiago Bernabeu majira ya kiangazi.

Nahodha huyo wa Ubelgiji, alifunga bao dakika ya 16 baada ya kupewa pasi na Karim Benzema.

Hazard alicheza dakika 62, lakini winga Gareth Bale hakucheza mchezo huo ikiwa ni muendelezo wa uhusiano wake mbaya na Kocha Zinedine Zidane.

Hazard ametua Real Madrid kwa Pauni150 milioni na matarajio yake ni kucheza kwa kiwango bora.

Zidane alionekana akifurahia bao la Hazard na hakuonyesha kusikitika kumuacha benchi Bale.

Zikiwa zimebaki siku 10 kabla ya msimu mpya kuanza, Zidane ametumia mfumo 3-5-2 akiwapanga pamoja katika safu ya ushambuliaji Hazard na Benzima.

Katika mfumo huo, Zidane aliwatumia viungo watatu katika mchezo huo Toni Kroos, Isco na Casemiro.