Kashasha, Mwaisabula waukubali muziki wa Simba, Yanga

Muktasari:

Msimu huu mechi ya Simba na Yanga itakuwa kali kabisa tofauti na msimu uliopita ambapo Yanga walionekana kuwa zaidi kuliko watani zao, na yote hato ni kutokana na usajili mzuri ambao umefanyika katika timu zote mbili.

Dar es Salaam.Mechi mbili za Kimataifa za kirafiki kati ya Simba na Power Dynamos na Yanga dhidi ya Kariobang Sharks zimewaibua wachambuzi wa masuala ya soka nchini na kueleza viwango vya wachezaji wapya waliocheza katika vikosi hivyo vya timu zote mbili kongwe hapa nchini.

Kocha wa zamani wa Yanga Kenny Mwaisabula, alisema amekiona kikosi cha Simba na Yanga haswa wale wachezaji wapya ambao waliosajiliwa na timu hizo na kubaini mambo ya msingi kutoka kwao kulingana na mapungufu ambayo waliyaonesha msimu uliopita.

Mwaisabula alisema katika kikosi cha Simba wachezaji Francis Kahata na Sharaf Eldin Shiboub, Deo Kanda ni miongoni mwa sajili bora ambazo zimefanywa na timu hizo kulingana na walivyocheza katika mechi ya kwanza ya Kimataifa ya kirafiki.

"Simba wamezidi kuimalika katika maeneo mengi wamekuwa bora baada ya kufanya usajili wao na nawaona watakwenda kuwa bora na watafanya imara zaidi ya msimu uliopita katika mashindano yote ambayo watashiriki," alisema.

"Kwa upande wa Yanga babo wachezaji wao wapya hawapishani viwango sana na wale ambao walikuwa kwenye timu msimu uliopita, na katika mashindano ya Kimataifa ambayo wanakwenda kushiriki hawataweza kufanya vizuri moja kwa moja kutokana walikuwa nje ya mashindano kwa muda tofauti na Simba ambao wameonja radha ya mafanikio msimu uliopita.

"Katika mechi ya Simba na Yanga hata kama kuna timu ambayo inawachezaji wazuri waliokuwa katika viwango bora huwezi kusema utakuwa mchezaji wa aina gani na timu ambayo itaondoka na ushindi ni ile ambayo itajiandaa vizuri licha ya kwamba Simba wameonekana kuimalika zaidi," alisema Mwaisabula. 

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini Alex Kashasha, alisema msimu huu mechi ya Simba na Yanga itakuwa kali kabisa tofauti na msimu uliopita ambapo Yanga walionekana kuwa zaidi kuliko watani zao, na yote hato ni kutokana na usajili mzuri ambao umefanyika katika timu zote mbili.

Kashasha alisema katika msimu ambao usajili umeafanyika kwa nidhamu kwa maana ya kuzingatia matakwa ya benchi la ufundi ni huu kwani wachezaji wote wapya ambao walicheza katika mechi ya Simba na Yanga walionesha kuwa wanaviwango vizuri na wameziba kasoro za msimu uliopita.

"Usajili huu kutakuwa na mchuano mkali katika mashindano ya ndani kwa Simba na Yanga lakini hata katika mashindano ya Kimataifa ambayo wataanza kucheza mwisho wa wiki hii naziona timu zote kufanya vizuri kwani zimeimarika tofauti na msimu uliopita," alisema Kashasha.