Tanzanite yapoteza kwa Zambia mashindano ya Cosafa U20

Muktasari:

Licha ya kipigo hicho walichokipata kwenye mechi ya kukamilisha ratiba ya Kundi B iliyopigwa kwenye Uwanja wa Wolfson, uliopo mji wa Port Elizabeth, Tanzanite imefuzu nusu fainali ya michuano hiyo na sasa itavaana na wenyeji, Afrika Kusini Jumapili hii.

Dar es Salaam. Timu ya taifa ya Wanawake U20, Tanzanite imepoteza mechi ya kwanza kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika kwa Wanawake (Cosafa Women U20) mchana huu kwa kufungwa mabao 2-1 na Zambia.
Licha ya kipigo hicho walichokipata kwenye mechi ya kukamilisha ratiba ya Kundi B iliyopigwa kwenye Uwanja wa Wolfson, uliopo mji wa Port Elizabeth, Tanzanite imefuzu nusu fainali ya michuano hiyo na sasa itavaana na wenyeji, Afrika Kusini Jumapili hii.
Katika mchezo huo uliopigwa saa 7 mchana wa leo Jumanne, Wazambia waliomaliza kama vinara wa kundi hilo walianza kuandika bao dakika ya ne tu ya mchezo kupitia kwa straika wake, Florence Kasonde na kabla ya Christine Kalange kuongeza bao la pili dakika ya 61.
Hata hivyo dakika sita kabla ya pambano kumalizika, Enekia Kasonga aliipatia Tanzanite bao ka kufutia machozi na kuifanya timu hiyo iliyoalikwa tu kwenye michuano hiyo kumaliza nafasi ya pili ikiwa na alama sita na mabao 11 ya kufunga na kufungwa mawili tu.
Mwishoni mwa mwaka jana timu ya taifa ya Vijana U17, Serengeti Boys ikialikwa kwenye michuano hiyo kama hiyo, ilitwaa ubingwa wa michuano ya ukanda huo wa CosafaU17 kwa kuinyoosha Angola.