Kikeke atoboa kilichoighalimu za Tanzania ‘Taifa Stars’ Afcon 2019

Muktasari:

Kimsingi mataifa mengi ya Afrika Magharibi yana bajeti kubwa zinazoruhusu ujenzi wa miundombinu na kununua wachezaji bora

Dar es Salaam. Ng'ombe wa masikini hazai, ni msamiati sahihi unaoakisi hali ya Taifa Stars baada ya kupenya kwa ‘hesabu za vidole’ ilipofuzu fainali za Afcon 2019 huku ikijikuta katika kibarua cha kundi C, ikitakiwa kusonga mbele katikati ya miamba wawili, Senegal na Algeria, waliocheza fainali siku nne zilizopita.

Fainali hizo za michuano ya kandanda ya mataifa ya Afrika nchini Misri, Algeria ilishinda kombe hilo kwa mara ya pili baada ya kuifunga Senegal bao 1-0.

Kwa hapa nchini michuano hiyo iliibua hisia tofauti kupitia amsha amsha ya uhamasishaji wa kuiunga mkono Stars, lakini hadi michezo mitatu inamalizika Tanzania ilipoteza mechi zake tatu kwa kufungwa jumla ya mabao nane.

Katika mahojiano maalumu na Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Salim Kikeke aliyeshuhudia michuano hiyo anaeleza wazi ilitegemewa maajabu Taifa Stars kutoka salama katika kundi C.

 

Anasema baada ya Taifa Stars kutocheza Afcon kwa miaka 39, kurejea na kupangwa katika kundi hili ilikuwa ni kama msemo “kubatizwa kwa moto”. Anasema Algeria na Senegal ni timu zilizoizidi Taifa Stars kwa ‘hali na mali.

“Senegal walicheza Kombe la Dunia Urusi mwaka 2018. Kwenye orodha ya FIFA ya Juni 2019 Senegal iko namba 22. Algeria licha ya kutofuzu Kombe la Dunia mwaka 2018, ilishinda Afcon 1990, ilikuwa timu ya kwanza Afrika  kufunga magoli manne Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Korea Kusini., kwa hiyo uzoefu wa mataifa hayo mawili ikilinganishwa na Tanzania tofauti ni kubwa.”

 

Mwandishi: Tatizo la Stars linaanzia wapi?

Kikeke: Timu zote ambazo zimepata mafanikio duniani zimetumia mambo kadhaa makuu ikiwemo uwekezaji katika soka na mipango thabiti.

Tukitazama mfano mdogo wa uwekezaji katika mataifa ya Afrika Magharibi, bajeti ni zaidi ya dola 10 milioni hutumika katika vilabu tu. Wydad Casablanca ya Morocco mathalan, msimu uliopita ilitengeneza dola 12 milioni huku Esperance ya Tunisia ikitangaza bajeti ya dola 8.5 milioni katika msimu wa 2015/16.  Klabu ‘mpya’ kama Pyramids FC ilitumia zaidi ya dola 50 milioni katika usajili.

Katika maeneo yetu ukanda wa Afrika Mashariki, pengine TP Mazembe ya DR Congo imeonyesha kuwa uwekezaji ni jambo muhimu. Kimsingi mataifa mengi ya Afrika Magharibi yana bajeti kubwa zinazoruhusu ujenzi wa miundombinu na kununua wachezaji bora.

Lakini unaposhuka chini zaidi kwa Tanzania unakutana na viwanja visivyo na ubora wa kutosha. Na mipango ya timu lazima ifahamike ni ipi. Lazima kuwe na malengo na tahmini yakinifu ya kufikiwa au kutofikiwa na baadaye kuona mwelekeo upi wa kuchukua.

Senegal ambayo imecheza fainali, imekuwa na meneja wake Alliu Cisse kwa miaka minne.  Aliwapeleka Simba wa Teranga kwenye Kombe la Dunia baada ya miaka 16, na kuipeleka Senegal kwenye fainali ya Afcon baada ya miaka 17.  “Haya ni matunda ya maandalizi ya muda mrefu” alisema Cisse.

Mpira ni pesa, unavyowekeza fedha nyingi zaidi ndio uwezekano wa kupata mafanikio zaidi unaongezeka.

 

Mwandishi: Jambo gani binafsi lilikugusa katika michuano hii?

Kikeke:  Kubwa lilikuwa kusikia wimbo wa Taifa ukipigwa kwenye michuano hii mikubwa. Ni kama ndoto. Nimetangaza Kombe la Mataifa mara nyingi na hata Kombe la Dunia, na nyimbo za taifa zikipigwa inakuwa kama sehemu tu ya kazi yangu, lakini safari hii nilihisi kitu tofauti kabisa. Hisia ambazo huwezi kuziweka kwenye maneno.

Hali kadhalika kupata nafasi ya kutangaza mpira wa kimataifa ambao unahusisha Taifa Stars ni jambo nitakalo lienzi milele.

 

Mwandishi:Pamoja na utofauti huo,mambo yaliyotokea lakini hayakutangazwa sana

Kikeke: Joto la Misri. Pamoja na kuwahi kuishi Dar es salaam, joto la Misri lilikuwa sio mchezo. Inawezekana joto huenda ikawa moja ya sababu ya mechi kutokuwa na magoli mengi, kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi.

 

Usalama ulikuwa wa hali ya juu kabisa. Kwenye mchezo wa fainali takriban polisi na wanajeshi 2000 walikuwepo ndani na nje ya uwanja wa Cairo International wenye uwezo wa kubeba watu 75,000 kuhakikisha mashabiki hawapati rabsha zozote.

Licha ya mchezo wa fainali kuwa ‘doro’ kwa Afrika ni hatua nzuri kwa kuwa Senegal na Algeria zilozocheza fainali hiyo zote zinafundishwa na makocha vijana wa Afrika.

Kwa mashabiki, wengi walipata tatizo la kuingia uwanjani kutokana na mfumuo wa ununuaji tiketi wa kutumia mtandao wa intaneti.

 

Mwandishi: Tathmini yako ya ujumla ya Afcon

Kikeke: Ilikuwa michuano yenye changamoto kadhaa tangu mwanzo. Misri walilazimika kuwa wenyeji baada ya Cameroon kutokuwa tayari. Ilikuwa kwa mara ya kwanza Afcon inashirikisha timu 24.

Na kwa mara ya kwanza mashindano haya yalifanyika Juni na Julai tofauti na Januari na Fenruari. Misri waliweza kukabili yote hayo na kufanya michuano hii kuwa na mafanikio kwa ujumla.

 

Tayari walikuwa na viwanja vya kutosha kwa ajili ya mechi, na viwanja vya kutosha kwa kila timu kufanyia mazoezi. Kulikuwa na hoteli nzuri na za kutosha kwa timu na hata mashabiki, jambo ambalo huwa changamoto katika michuano kama hii kwa baadhi ya nchi wenyeji.

Uwanjani michuano hii haikuwa na msisimko mkubwa na hatukushuhudia kandanda la kuvutia isipukuwa katika mechi kadhaa. Pengine mechi pekee ya kusisimua zaidi katika michuano hii ilikuwa kati ya Kenya na Tanzania katika kundi C, tulishuhudia magoli, mpira ukitandazwa na ari ya ushindi.  

Ni mechi ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na mataifa haya jirani na kimchezo haikuwaangusha mashabiki ingawa matokeo yaliumiza mashabiki wa Taifa Stars, lakini soka lilipigwa inavyotakiwa.