Majembe ya hatari, usajili umedoda tu

Muktasari:

Pazia la dirisha la uhamisho la Uingereza linafungwa Agosti 8. Kwa hiyo, walio na mpango wa kusajili, wamebakisha takribani siku 19 tu kufanya hivyo.

TOFAUTI na miaka ya nyuma, Ligi Kuu ya England msimu huu haijashuhudiwa usajili wa kutisha ukifanyika katika dirisha la usajili linaloendelea. Huko nyuma tumeshuhudia klabu kubwa zikitoana jasho kugombania saini za wachezaji nyota, lakini safari hii kimya kimetawala.
Aidha, katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na mtindo wa kusaini mabeki imara, tena kwa gharama kubwa sana, mbinu ambayo msimu uliopita ilionekana kulipa kwa klabu kama Liverpool na Manchester City.
Pazia la dirisha la uhamisho la Uingereza linafungwa Agosti 8. Kwa hiyo, walio na mpango wa kusajili, wamebakisha takribani siku 19 tu kufanya hivyo.  Wakati tukisubiri sarakasi za dakika za mwisho za usajili, tuwaangalie wakali watano walionaswa mpaka sasa.

5. RODRI
– MANCHESTER CITY
Pep Guardiola alikuwa anahitaji kumpata mrithi wa Fernandinho kwa gharama yoyote ile. Kazi ya kumpata mchezaji sahihi haikuwa kazi rahisi kwa sababu wachezaji wa aina ya Fernandinho ni wachache pia.
Hata hivyo, baada ya kupekua pekua, hatimaye Mhispania huyo alikutana na Rodrigo. Hakuchukua muda baada ya kumshuhudia akicheza, fasta akamwaga fedha na kumvuta Etihad.
Unaweza ukashangaa ni kitu gani kilichomvutia Pep kwa kiungo huyu.
Kwa waliopata bahati ya kumshuhudia uwanjani, watakubaliana na Guardiola kuwa, huyu ni pacha wa Sergio Busquets, Rodri ana kila sababu ya kuwa kiungo bora duniani baada ya miaka mitano. City walimchukua kwa pauni 70 milioni kutoka Atletico Madrid.

4. CHRISTIAN PULISIC
– CHELSEA FC
Licha ya usajili wake ulifanyika katika majira ya kiangazi ya mwaka jana, ilikuwa dhahiri kuwa Mmarekani Christian Pulisic angelazimika kusubiri hadi msimu mpya uanze kabla ya kuruhusiwa kujiunga na Chelsea.
Straika huyu anatazamiwa na wengi kuvaa viatu vya Eden Hazard, aliyejiunga na Real Madrid, pamoja na rekodi kuonesha kuwa bado ana safari ndefu kumfikia Mbelgiji huyo, lakini kitu kizuri ni kwamba anaouwezo wa kuja Stamford Bridge na kuandika historia na ufalme wake mwenyewe.
Hakuna uwezekano wa nyota huyo kufanikiwa klabuni hapo kama atakuja Darajani akiwa na mawazo ya kuziba pengo la mtu kwa sababu rekodi zake uwanjani zinaonesha kuwa ana uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa kwenye EPL.

3. TANGUY NDOMBELE
– TOTTENHAM
Kiungo wa zamani wa Olympique Lyonnais, Tanguy Ndombele, ni mmoja wa nyota waliotikisa dirisha la usajili akigombaniwa na klabu nyingi kubwa Ulaya.
Zidane alikuwa na mpango wa kumpeleka Santiago Bernabeu lakini ni Pochettino aliyefanikiwa kumshawishi.
Hatimaye akaoneshwa njia ya kuelekea London ambapo amesajiliwa katika klabu ya Tottenham Hotspurs kwa dau la pauni 60 milioni na kumfanya nyota wa kwanza aliyesajiliwa na klabu hiyo yenye maskani yake London Kaskazini. Mfaransa huyu ni anakaba hadi kivuli.

2. RAUL JIMENEZ
– WOLVERHAMPTON WANDERERS
Baada ya kuonesha uwezo mkubwa kwenye kikosi cha Wolverhampton kwa mkopo hatimaye Raul Jimenez amefanikiwa kuwashawishi mabosi wa klabu hiyo kumpatia mkataba wa kudumu wakimnunua kutoka Benfica ya Ureno.
Mshambualiaji huyu raia wa Mexico anatajwa kuwa ni kiungo bora anayetokea katika klabu ambayo haiko kwenye sita bora ya EPL.
Msimu uliopita, Jimenez alizifunga klabu zote za Top Six na anaonesha dalili ya kuwa mmoja wa viungo bora duniani katika siku za usoni.

1. PABLO FORNALS
– WEST HAM UNITED
Hii inaweza ikaonekana kama kampeni lakini ukweli ni kwamba, kocha Manuel Pellegrini, ana uelewa mkubwa sana wa Akademi za klabu ya Villarreal na Malaga. Huamini? Kocha huyu raia wa Chile alizifundisha klabu hizi huko nyuma kabla ya kuhamia kwenye EPL.
Katika safari na maisha yake ya ukocha huko Hispania alikuwa makini sana kuwafuatilia baadhi ya wanasoka makinda; Pablo Fornals, akiwa ni mmoja wao.
Akiwa na umri wa miaka 23, ni wazi kuwa usajili wa Fornals ndio usajili bora kabisa uliofanyika mpaka sasa.
Jina lake linaweza likawa ngeni katika masikio ya wengi, lakini amini usiamini Fornals atawaacha wengi midomo wazi msimu utakapoanza. Najua wengi hawaamini ikizingatia kuwa anaenda katika klabu ya kawaida.  Tukutatane Agosti 10, shughuli ikianza!