Kakolanya, Gadiel watema cheche Simba

Muktasari:

Mwanaspoti limeweka kambi nchini humu kukupasha habari moto moto kila ambacho kinajiri mwanzo mpaka mwisho wa kambi, ambapo nyota wapya wawili waliosajiliwa kutoka Yanga kipa Benno Kakolanya na beki Gadiel Michael wametema cheche zao.

KIKOSI cha Simba kinaendelea na mazoezi ya msimu ujao Afrika Kusini huku kila mchezaji akionesha kuwa na morali ya hali ya juu kuonesha ubora katika kila zoezi ambalo hupatiwa na walimu wa timu hiyo.
Mwanaspoti limeweka kambi nchini humu kukupasha habari moto moto kila ambacho kinajiri mwanzo mpaka mwisho wa kambi, ambapo nyota wapya wawili waliosajiliwa kutoka Yanga kipa Benno Kakolanya na beki Gadiel Michael wametema cheche zao.
Kakolanya aliyetua akikutana na upinzani kutoka kwa Aishi Manula aliyekuwa na misimu miwili yenye mafanikio Msimbazi, alidai anaujua ubora wa mwenzake katika kulinda lango akinyakua tuzo ya kipa bora wa msimu mara mbili mfululizo, amekuwa chaguo la kwanza katika kikosi hicho kwa muda mrefu lakini hata katika timu ya Taifa ni hivyo.
“Kwanza ambacho nitakifanya ni kumpa heshima kutokana na utawala wake, pili nitakuwa najifunza ubora aliokuwa nao ili niweze kufikia hapo alipo,” alisema.
“Nikiwa nafanya vizuri katika mazoezi, nina imani nitapata nafasi ya kucheza katika mchezo hata mmoja na kwa kuwa nitakuwa na vitu vingi nimevipata kutoka kwa walimu na kipa mwenzangu, nina imani nitafanya vyema.
“Mpaka Simba wameamua kunileta hapa basi nina imani nina uwezo na ni jambo ambalo litaongeza ushindani wa namba hapa. Benchi la ufundi litaamua kipa ambaye atacheza,” alisema Kakolanya.
Naye Gadiel alisema mpaka anafanya uamuzi wa kujiunga na Simba alifahamu ataenda kukutana na ushindani wa namba kwa maana ya kuwania nafasi ya kucheza.
Gadiel alisema anafahamu kuwa Tshabalala ni miomgoni mwa mabeki wa kushoto bora waliopo nchini kwa sasa, na hilo ni jambo linalomfanya kutokubweteka hata kidogo.
“Ushindani wetu si hapa Simba mbali hata katika timu ya Taifa na tulikuwa tukicheza kwa kupishana kwa maana hiyo naamini hata hapa kuna ambaye atakuwa chaguo la kwanza na mwingine atakuwa mbadala wa mwenzake au tutacheza kwa kupishana,” alisema.
“Kwangu nitafanya kila ambalo natakiwa na benchi la ufundi kulifanya tukiwa mazoezini na hata kwenye mechi huku nikiwa na imani kubwa ya kucheza mara kwa mara, lakini makocha ndiyo wenye uamuzi wa mwisho,” alisema Gadiel beki huyo aliyetokea Yanga.