Shilton amaliza utata wa vita ya makipa Simba

Muktasari:

Shilton alisema kutokana na namna ushindani uliopo kwa makipa wake, Aishi Manula, Beno Kakolanya na Salim Ally inaonyesha kazi itakuwa kubwa katika vita ya kuwania nafasi ya kukabidhiwa dhamana ya kuliongoza jahazi la Msimbazi msimu ujao

KOCHA wa makipa, Mohammed Muharami ‘Shilton’ amevunja ukimya na kumaliza utata wa makipa wake watatu alionao kambini nchini hapa, akisema mpaka sasa hakuna mwenye uhakika wa kuwa namba moja mpaka wapimwe kwenye mechi za mashindano.
Shilton alisema kutokana na namna ushindani uliopo kwa makipa wake, Aishi Manula, Beno Kakolanya na Salim Ally inaonyesha kazi itakuwa kubwa katika vita ya kuwania nafasi ya kukabidhiwa dhamana ya kuliongoza jahazi la Msimbazi msimu ujao.
Kakolanya ni usajili mpya msimu huu kutoka Yanga na Manula alikuwepo tangu awali na ndiye alikuwa namba moja akimweka Deogratius Munishi ‘Dida’ benchi.
“Kuna ushindani lakini kati ya wao wote lazima apatikane namba moja wa timu kulingana na aina ya soka la kimataifa. Huwezi kuwachezesha makipa wote wakawa wanapokezana, ndio mpira wa kisasa,” alisema Shilton.
Alisema, anayefanya kazi nzuri ndiye atakayepewa nafasi hiyo na ataonekana katika mechi za mashindano lakini si za majaribio.
“Mtamwona tu huyo namba moja wa Simba, ushindani ni mkubwa kwani pamoja na Kakolanya ameingia akiwa mgeni, anachofundishwa amekuwa akikishika vizuri.”
Alimzungumzia Dida na kusema, alikuwa kipa mzuri lakini kama alivyosema awali, ni mipango tu ambayo inapangwa. Pia, alisema jambo jingine kuhusu Dida ni kwamba alimaliza mkataba wake na hakuongezewa mpya.