Kipa Kisu ajilaumu kuchelewa kucheza soka la kulipwa

Muktasari:

Kama kuna kitu amejifunza David Kisu baada ya kujiunga na Gor Mahia ya Kenya ni kuona alichelewa kufanya uamuzi ya kwenda mapema kucheza soka la kulipwa nje.

Dar es Salaam. Kipa mpya wa Gor Mahia, David Kisu amesema ameona kama alichelewa kufanya uamuzi ya kutoka kwenda kucheza nje.

Kisu amejiunga na Gor Mahia ya Kenya kwa mkataba wa miaka mitatu, akitokea Singida United, alisema kwa maisha anayoishi nchini humo anajilaumu kwa nini hakuanua mapema kucheza nje.

Alisema amebaini utofauti mkubwa wa wachezaji wa Kenya wanavyochukulia kazi ya soka kwa upana wake, akidai tofauti na hapa Tanzania.

"Tanzania kuna vipaji vikubwa ila ni baadhi wanaothamini kazi yao ndio wale ambao viwango vyao haviyumbi, lakini Kenya wana juhudi inayowafanya waonekane wapo juu.

"Nidhamu ya kazi ni jambo linalopewa nafasi kubwa, kwa maana ukifika muda wa mazoezi hakuna mchezaji anayeweza kuonyesha masihala kila mmoja anajituma ili kumshawishi kocha."

"Hakuna mambo ya kujiona staa wakati wa kazi, napamba kwa kadri niwezavyo ili kocha aweze kuona nilichonacho ili ligi ikianza Agosti niweze kuanza kwenye kikosi cha kwanza," alisema Kisu.