Ndayiragije: Bahati haikuwa upande wetu Kagame Cup

Dar es Salaam. Kocha mkuu wa Azam, Etienne Ndayiragije amesema hawakuwa na bahati ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame walipocheza fainali jana na KCCA nchini Rwanda.

Akizungumza na MCL Digital muda mfupi baada ya kurejea nchini Leo Jumatatu, kocha huyo ameiongoza Azam kwa mara ya kwanza tangu alipoajiliwa hivi karibuni alisema walifanya makosa madogo ambayo yaliwagharimu hadi kupelekea kukosa ubingwa.

"Vijana walicheza vizuri, walimiriki mipira kwa asilimia kubwa, lakini bahati haikuwa upande wetu, kosa dogo limetugharimu tumekosa ubingwa," alisema kocha huyo.

Alisema licha ya kukosa ubingwa, lakini mashindano ya Kgame yamekuwa kipimo kizuri kwao katika maandalizi ya kuelelekea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Lengo mbali na ubingwa ambao tumeukosa, lakini pia nilihitaji kutengeneza kikosi kipana ndiyo sababu mbali na timu ya wakubwa tulikwenda na timu B ya vijana chini ya miaka 20," alisema kocha huyo.

Alisema ameyatumia mashindano ya Kagame kama fursa ya kutengeneza kikosi kipana na vijana aliokwenda nao wamepata uzoefu wa kutosha.

Alisema kingine kilichowasumbua ni kanuni za Cecafa kwenye mashindano yale hasa kwa timu ambazo hazikuwa na maandalizi ya kutosha.

"Kila timu ilitakiwa isajili wachezaji 20 na makipa watatu, bahati mbaya katikati ya mashindano wachezaji wangu baadhi wakapata majeruhi sikuweza kuwatumia, hivyo nikalazimika katika mechi kubaki na wachezaji 15 pekee ambao walicheza mwanzo mwisho," alisema Mrundi huyo.