Edo Christopher aikacha Kagera Sugar atua Ruvu Shooting

Muktasari:

Baada ya Christopher Edward kuisaidia Kagera Sugar isishuke daraja msimu ulioisha, msimu ujao atakuwa na Ruvu Shooting baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Christopher Edward 'Edo' atavaa uzi wa Ruvu Shooting kwa msimu ujao baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja akitokea Kagera Sugar.

Edo ameiambia Mwanaspoti Online amejiunga na Ruvu Shooting itakayokuwa chini ya kocha Salum Mayanga ili kusaka changamoto mpya ya kisoka.

Alisema amejifunza vitu vingi vya kiufundi akiwa chini ya kocha Mecky Maxime wa Kagera Sugar, kwa sasa ataendelea kutaka kujua zaidi soka la kisasa kwa kocha wake mpya Mayanga.

"Soka kwangu ni maisha, hivyo nalazimika kujifunza kila siku, nilikuwa na Kagera Sugar msimu ulioisha, tukapambana kuhakikisha timu inabaki, imekuwa hivyo.

"Natamani kupata changamoto mpya kila msimu ili kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na lengo kubwa ni kuona nazifikia ndoto zangu kabla umri haujanitupa mkono.

"Tayari nimejiunga na Ruvu, kambini kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao, ambao natamani kufanya kitu cha tofauti sana kwenye ligi, naamini kwa kuzingatia mafundisho ya kocha nitafika mbali," alisema Edo.