Kwa bondia Mjerumani, Class akibugi imekula kwake

Muktasari:

Class bondia namba moja kwenye uzani wa super feather nchini amepigana mapambano 29, ameshinda mapambano 23 (11 kwa KO), amepigwa mara 6 (3 KO) hajawahi kutoka sare.

Dar es Salaam. Bondia bingwa wa zamani wa dunia wa Global Boxing Council (GBC), Ibrahim Class atapanda ulingoni kumkabiri Mjerumani, Sergej Vib Agosti 31 mkoani Iringa pambano la uzani wa super feather la raundi 10.

Bondia huyo Mtanzania amejiweka mtegoni endapo ataruhusu kupoteza pambano hilo atampa mwanya mpinzani wake kupanda kwenye viwango vya ubora kutokana na rekodi za wote wawili.

Class mwenye nyota mbili na nusu katika ubora wa ngumi atazichapa na Vib ambaye ana nusu nyota, rekodi ambayo kama ikitokea Vib ameshinda basi, Class anaweza kupoteza nyota zake kadhaa.

"Niko vizuri, najua ni pambano gumu ambalo Vib hana cha kupoteza, lakini anaweza kupanda mara dufu kama akishinda, hivyo hiyo ni zaidi ya vita kwangu," alisema Class anayenolewa na kocha Habib Kinyogoli (Master).

Alisema mpinzani wake ni bondia mzoefu mwenye rekodi nzuri, hivyo ili amkabiri lazima aongeze bidii katika mazoezi jambo ambalo analifanya sasa.

Mjerumani huyo ana rekodi ya kupigana mapambano 21 na kushinda 11 (8 kwa KO) amepigwa mapambano 10 (7 kwa KO) hajawahi kutoka sare.