Chirwa atoboa sababu ya Azam kuchapwa na KCCA

Muktasari:

Azam tayari imeshatua nchini ikitokea Rwanda baada ya kumaliza mashindano ya Kombe la Kagame na kuambulia nafasi ya pili baada ya kufungwa kwenye fainali.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Azam, Obrey Chirwa ameweka wazi sababu iliyowaangusha na kushindwa kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame ni kuzidiwa mbinu na wapinzani wao.

Azam FC wameshindwa kutetea taji lao baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa KCCA ya Uganda ambao pia waliwafunga katika hatua ya makundi.

Chirwa amesema KCCA wamewazidi uwezo na ndio maana wameshindwa kupata matokeo katika michezo yote miwili waliyokutana nao, lakini wamejifunza kitu kutoka kwao.

"Tumesharudi tangu saa kumi alfajili tupo kambini Chamazi tayari kwaajili ya kuendelea na maandalizi ya ligi ikiwa ni sambamba na mashindano ya kimataifa ambayo tayari ratiba yake imetoka."

"Siwezi kuizungumzia ratiba hiyo kwasasa kikubwa mashabiki wetu watambue kuwa tumeshaingia kambini kujiandaa kwaajili ya michezo mingine iliyombele yetu yaliyopita tumeshayasahau," alisema Chirwa.