Bilo aanza Alliance kwa kuangalia uwezo wa nyota wake

Muktasari:

Kocha mpya wa Alliance, Athuman Bilali 'Bilo' ameanza kuweka mipango sawa ndani ya kikosi chake ili kuhakikisha anakuwa na kombinesheni ya maana msimu ujao.

Dar es Salaam.Kocha mpya wa Alliance, Athuman Bilali 'Bilo' amesema anaanza rasmi kukikagua kikosi chake kwa kuangalia ubora na mapungufu ya wachezaji wake mapema.

Bilo msimu uliopita alikuwa na Stand United iliyoshuka daraja, amesema amekuta wachezaji wengi wamesajili jambo la kwanza katika mazoezi yake ya leo ni kuona uwezo wao.

Alisema lengo lake anataka kuwa na kikosi kitakachomsaidia kutimiza malengo ya timu hiyo kwa msimu ujao, jambo alilosisitiza kwamba lazima apate wachezaji wenye uwezo wa juu.

"Mazoezi ya leo yatakuwa yakujua aina ya wachezaji nilionao pia wao kunijua kocha wao, kuanza kuandaa mikakati ya kuhakikisha tunakuwa wapinzani wa kweli kwenye ligi kuu Bara.

"Kadri siku zitakavyokuwa zinaendelea nitakuwa natengeneza kombinesheni nzuri ya nani acheze na nani pia kama kutakuwa na ulazima wa baadhi kubadilisha namba zao.

"Mfano mzuri nilipokuwa na Stand United nilimbadilisha Jacob Masawe acheze mshambuliaji wa mwisho na sio kiungo kama alivyokuwa mwanzo na alifanya vizuri zaidi, naamini Alliance itakuwa na msimu mzuri ujao," alisema Bilo.