KCCA mabingwa wapya Kagame Cup yaichapa Azam FC

Muktasari:

Azam walishatwaa taji hilo mwaka 2015 na 2018 na jana kwenye mechi yao ya fainali iliyopigwa mjini Kigali, Rwanda ilikuwa ikisaka heshima ya Leopards iliyowekwa mwaka 1982-1983 na 1984.

Kigali, Rwanda.Mabingwa watetezi Azam FC imepoteza ubingwa wao wa Kombe la Kagame baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa KCCA ya Uganda katika fainali ya mashindano hayo.

Bao pekee la dakika ya 62 la Mustafa Kiiza wa KCCA lilitosha kuipeperusha ndoto za Azam FC kufikia rekodi ya AFC Leopards ya Kenya ya kubeba taji la michuano ya Kombe la Kagame kwa mara tatu mfululizo baada ya jana wawakilishi hao wa Tanzania kulala 1-0.

Azam walishatwaa taji hilo mwaka 2015 na 2018 na jana kwenye mechi yao ya fainali iliyopigwa mjini Kigali, Rwanda ilikuwa ikisaka heshima ya Leopards iliyowekwa mwaka 1982-1983 na 1984, lakini wakakutana na kikwazo kwam Waganda wanaobeba kwa mara ya pil baada ya taji lao la kwanza mwaka 1978.

Katika mchezo huo, Azam iliwabana vizuri KCCA ambao waliwatambia kwenye mechi ya makundi ya michuano ya mwaka huu, japo kipa wake, Razak Abarola alikuwa na kazi ya ziada kuokoa michomo mikali ya mabingwa hao wapya wa Kagame.

Hata hivyo makosa ya mabeki wa Azam yaliyomchanganya kipa wao, yalitosha kuwapa nafasi KCCA kuandika historia ya kulibeba taji hilo la pili kwao, huku kocha Etienne Ndayiragije aliwasifia washindi hao akidai makosa ya nyota wake yamewagharimu.

Katika mechji ya kusaka mshindi wa tatu, AS Maniema ya DC Congo walinyooshwa kwa kucharazwa mabao 2-0 na Green Eagles ya Zambia.

KCCA imevuna Kombe, Medali na Dola 30,000 (zaidi ya Sh 68 milioni) huku Azam ikizoa Dola 20,000 (zaidi ya Sh 45 milioni) na Wazambia waliambulia Dola 10,000.