Van Dijk: Nipeni tu Ballon d'Or yangu

Muktasari:

Kutokana na mambo hayo makubwa, Van Dijk kafunguka kwamba jambo alisema anatamani timu yake itwae taji la Ligi ya Mabingwa kuliko mtu kushinda tuzo binafsi, sasa kasema hata hiyo Ballon d’Or anaitaka.

BEKI wa Liverpool, Virgil van Dijk ameona hamna haja ya kuendelea kuyaweka moyoni. Amefunguka kwamba anaitaka hiyo tuzo ya Ballon d’Or.
Mholanzi huyo tayari ameshinda tuzo ya PFA ya Mwanmasoka Bora wa Mwaka kutokana na kiwango chake kilichowapa Liverpool ndoo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuisaidia timu kumaliza katika nafasi ya pili ya Ligi Kuu ya England.
Kutokana na mambo hayo makubwa, Van Dijk kafunguka kwamba jambo alisema anatamani timu yake itwae taji la Ligi ya Mabingwa kuliko mtu kushinda tuzo binafsi, sasa kasema hata hiyo Ballon d’Or anaitaka.
“Kushinda tuzo PFA ya Mchezaji Bora wa Mwaka ni heshima kubwa,” Van Dijk aliiambia tovuti ya Liverpool, “Ni heshima kubwa kwa sababu unapigiwa kura na wachezaji wenzako wa kulipwa.
“Nilisema kule nyuma kwamba nachagua kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko tuzo binafsi.
“Lakini ni heshima pia watu kukuzungumzia kuhusu Ballon d’Or, lakini nitafanyaje? Sina ushawishi katika lolote.

“Siwezi kukataa kwamba nimekuwa na msimu mzuri sana, hivyo jambo pekee ninaloweza kufanya sasa ni kuweka akili katika msimu mpya, kuwa fiti, kuepuka majeraha na natumai nitakuwa na msimu bora kuliko uliopita.
“Natambua kwamba kwa kawaida mastraika au Namba 10 ndio huwa wanashinda tuzo hizi na ndiyo inavutia zaidi kuona. Lakini pengine muda wa mabadiliko umekuja.”
Beki wa mwisho kushinda Ballon d’Or alikuwa Fabio Cannavaro 2006.