Kaseja apewa zawadi kwa kuitwaa Taifa Stars

Muktasari:

Kaseja amepawa zawadi ya jezi chini na juu, mpira, glovu na kikombe kutambua mchango wake katika soka

Dar es Salaam. Kipa wa KMC, Juma Kaseja amepewa zawadi ya vifaa vya michezo ikiwa ni pongezi kwake kwa kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania baada ya kukaa nje kwa zaidi ya miaka mitano.

Kaseja nahodha wa KMC ametwaa katika kikosi cha Taifa Stars kinachojianda na mchezo dhidi ya Kenya wa kusaka kufuzu kwa fainali za CHAN 2021 Cameroon.

Baada ya Kaseja kupata nafasi hiyo kampuni ya kuuza na kusambaza vifaa vya michezo ya Justfit iliyopo Sayansi hapa Dar es Salaam kupitia Mkurugenzi wake Justfit Lutfi Islam imetoa zawadi kwa kipa huyo.

Islam alisema wamempa zawadi ya jezi chini na juu, mpira, glovu na kikombe ambacho wamempatia Kaseja kutambua mchango wake katika soka kwani amecheza kwa muda mrefu licha ya magumu ambayo amepitia bado yupo katika kiwango kizuri kama alivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Islam alisema kilicho wasukuma kingine uongozi wa kampuni yao ni kuona kipa huyo amejumuishwa tena katika kikosi cha Stars ambacho kitacheza mchezo wa kufuzu fainali za CHAN, ambazo zitakwenda kufanyika nchini Cameroon mwaka ujao.

"Tunaendelea kuwapa nguvu wachezaji wa zamani ambao bado wanafanya vizuri kwa kuwapa vifaa kutoka hapa Justfit, ili kutambua mchango wao na si tumefanya hivi kwa Kaseja bali tulifanya kwa Shaban Nditi wa Mtibwa Sugar na tunaendelea kwa wengine siku za usoni," alisema Islam.

Kaseja alisema tangu ameanza kucheza soka katika ngazi za juu 2001, hakuwai kupata zawadi kama hiyo ya kampuni binafsi kwa kutambua mchango wake ambao anautoa katika soka kwa muda alioanza kucheza mpaka wakati huu.

"Nashukuru kwa zawadi hii kubwa kwangu lakini namuahidi aliye nipatia kuna jambo kubwa ambalo nitakwenda kulifanya dhidi yake kama kulipa fadhira kwa jambo hili kupitia vifaa hivi ambavyo leo nimepewa," alisema Kaseja ambaye alikuwa akikabiziwa vifaa hivyo na kipa wa zamani wa Simba Iddi Pazi.