Nyuma ya Pazia: Mourinho, kama fisi na mkono wa mwanadamu

Muktasari:

Mara ya mwisho watu wa Forbes walituambia Jose ana utajiri wa Dola 50 milioni. Sawa, hakuna mwanadamu ambaye anaridhika na pesa, lakini Jose ataenda kuchukua pesa za akina Jiayn kama akimaliza hasira zake Ulaya.

KAMA mkono wa mwanadamu na fisi hivi. Fisi anatembea nao kwa zaidi ya kilomita moja akimiani kwamba utaanguka halafu atautafuna. Bahati mbaya hauanguki. Labda kama mwanadamu akiangushwa na simba. Hauanguki kirahisi.
Ni maisha anayoishi Jose Mourinho sasa hivi. Wiki mbili zilizopita alikutana na bilionea wa Kichina,Xu Jiayn anayemiliki klabu ya Guangzhou  Evergrande ya Ligi Kuu ya China. Amekataa ofa ya mshahara wa Euro 100 milioni. Kwa mwaka angechukua Euro 28 milioni.
Hakuna kocha aliyewahi kulipwa pesa hizo duniani. Hakuna. Jose akakataa. Kwanini? Tangu Desemba mwaka jana anatembea na hasira. Anatembea na kinyongo. Usidhani amechukulia poa baada ya kufukuzwa na Manchester United.
Kama pesa Jose anazo. Mara ya mwisho watu wa Forbes walituambia Jose ana utajiri wa Dola 50 milioni. Sawa, hakuna mwanadamu ambaye anaridhika na pesa, lakini Jose ataenda kuchukua pesa za akina Jiayn kama akimaliza hasira zake Ulaya.
Hasira zake zinakuja wapi? Jose bado anamendea kazi ya maana katika klabu ya maana pale Ulaya. Ana hasira. Anataka kuthibitisha kwamba yeye bado ni kocha yuleyule ambaye tulimfahamu na kumpenda. Chelsea na Manchester United zimemdhalilisha katika miaka ya karibuni.
Ndio maana Jose amekataa kazi China. Kazi ya pesa ndefu kutoka kwa tajiri JIayin ambaye ana utajiri wa Dola 31 bilioni. Weka hesabu vizuri hapa. Jose ana utajiri wa Dola 50 milioni, Jiayin ana utajiri wa Dola 31 bilioni. Tofauti kati ya milioni na bilioni.
Jose anaamini kazi nzuri bado zipo Ulaya. Anaamini kufika Septemba hadi Desemba kuna makocha watafukuzwa kazi. Sawa, itakuwa ngumu kurudi Manchester United hata kama Ole Gunnar Solskjaer akifukuzwa. Itakuwa ngumu kurudi Chelsea. Alishavunja daraja kwa kutengeneza uhusiano mbovu na mashabiki wakati akiwa Old Trafford.
Lakini kuna kazi anaziona. Vipi Unai Emery akifukuzwa na Arsenal? Vipi Thoma Tuchel akifukuzwa na PSG? Vipi kama Zinedine Zidane akirudi ovyo na kufukuzwa na Real Madrid baada ya matanuzi yote aliyofanya katika dirisha hili?
Vipi kama Niko Kovac akifukuzwa na Bayern Munich? Lakini vipi pia hata mambo yasipoenda sawa kwa Maurizio Sarri pale Juventus? Jose anasubiri kazi hizi kubwa kubwa. Amekataa ofa ya China lakini pia amekataa ofa ya Newcastle United.
Alipoikataa ofa ya Newcastle nilicheka kidogo. Alidai kwamba hawezi kukubali kwenda kuifundisha timu ambayo inafurahi kumaliza nafasi ya tisa. Hii ina maana kwamba Jose anajua kuwa anataka kuendelea kufundisha Ulaya lakini katika timu kubwa.
Anaishi kwa imani ileile ambayo fisi anaishi nayo dhidi ya mkono wa mwanadamu. Lakini hapo hapo piga hesabu za vidole. Unaamini kwamba wote hawa watasalimika kufikia Desemba? Maisha yanakwenda kasi siku hizi.
Usimuone Jose yupo kimya. Alishaingia katika wazimu wa mpira. Anajua kwamba sasa hivi angekuwa Marekani, China, Australia, Singapore au kwingineko akiiandaa moja kati ya timu kubwa barani Ulaya kwa ajili ya msimu mpya wa michuano mbalimbali.
Ana hasira na hili jambo. Hata hivyo mpaka sasa ameishia kunawa ingawa anatamani kula. Anachukia kukaa juu ya makochi ya vituo vya televisheni na kuitwa mchambuzi. Anachukia kufanya kazi ambayo yeye mwenyewe huwa anaichukia watu wakiifanya dhidi yake. Anataka awe pembeni ya mstari wa uwanja akibishana na mwamuzi wa akiba au kocha wa timu pinzani.
Ikitokea timu kubwa ikamfukuza kocha, ikamuahidi Jose mshahara mzuri na pesa nzuri ya uhamisho wa wachezaji, atarudi kazini haraka. Simuoni Jose akifundisha China, Marekani au timu ya taifa. Simuoni Jose mwenye kiu ya pesa.
Namuona Jose mwenye hasira ambaye amefukuzwa na timu mbili kubwa za England huku akiwa bado anaamini kwamba yeye ni kocha bora kuliko Pep Guardiola, Diego Simeone, Jurgen Klopp, Zidane na wengineo wengi wa kizazi hiki.
Anadai kwamba amepokea ofa nyingi kutoka klabu mbalimbali. Naamini hizo timu zote ambazo zilimfuata Jose zipo katika hadhi ya Newcastle. Labda akina Burnley, au Valencia ama Stuttgart. Jose hataki timu hizo wala wa za mabara mengine. Ana timu zake za kuthibitisha ubabe wake katika soka la Ulaya.
Na sisi watu wa nyuma ya pazia tunamsubiri Jose. Hatujui akirudi atarudi na mbinu gani mpya. Hatujui. Sijui ataendelea kugombana na mastaa au ataacha. Sijui atabadilika katika masuala yanayohusu menejimenti kwa ujumla. Sijui atabadilisha mbinu zake za soka uwanjani kwa kiwango cha juu. Yote haya hatujui isipokuwa tunamsubiri kwa hamu Jose.
Kwa sasa mwache aendelee kufukuzana na ‘mkono wa mwanadamu’, mwache aendelee kuwa fisi mzuri tu. Ikifika Desemba mwaka huu itakuwa mwaka mmoja bila ya Jose kazini. Lakini siamini kama atafika. Lazima hapo kati kuna kocha wa timu kubwa atafukuzwa.