Taifa Stars ya Ndayiragije fresh, makundi AFCON mipango tu!

Muktasari:

Moja ya mikakati hiyo ni benchi hilo jipya la ufundi lililoteuliwa chini ya Kocha Etienne Ndayiragije ni kufanya mabadiliko ya kikosi chake kwa kupunguza baadhi ya nyota waliokuwemo na kuongeza baadhi ambao hawakuwemo kwenye kikosi kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).

TUNA wiki moja imesalia kabla ya mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).
Tumeanza kuona mikakati mbalimbali ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na benchi la ufundi la timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kujiandaa na mechi hiyo ya kwanza nyumbani ambayo tutacheza na Kenya, Julai 28.

Moja ya mikakati hiyo ni benchi hilo jipya la ufundi lililoteuliwa chini ya Kocha Etienne Ndayiragije ni kufanya mabadiliko ya kikosi chake kwa kupunguza baadhi ya nyota waliokuwemo na kuongeza baadhi ambao hawakuwemo kwenye kikosi kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).
Kwa maoni yangu, kikosi ni kizuri na hakina shida kwa sababu kocha ametazama baadhi ya mambo ya msingi katika uteuzi wake.
Uteuzi ulionifurahisha zaidi ni wa kipa Juma Kaseja ambaye kwa sasa anadakia KMC iliyotoka kushiriki Mashindano ya Kombe la Kagame huko Rwanda.
Kaseja ni kipa mwenye quality (ubora) na uzoefu ambao bila shaka umemshawishi kocha Ndayiragije kumjumuisha kikosini.
Ni suala lisilopingika kwamba Kaseja ni kipa aliye kwenye kiwango bora kwa muda mrefu na uzoefu alionao utamsaidia kocha na timu kwani atakuwa kiongozi mzuri kwa wenzake ambao wengi wao amewaacha mbali kiumri.
Kwa ujumla kikosi kina ‘balance’ (uwiano) na sio kibaya kwa sababu kina kundi kubwa la wachezaji waliotoka kushiriki AFCON.
Na hata wale walioongezwa ni matokeo ya kitu kinaitwa ‘coaching style’ au Philosophy’ (staili ya ufundishaji na Falsafa) ya kocha. Kila kocha ana falsafa zake na aina ya wachezaji ambao anaamini wanaweza kuifanyika kazi staili yake ya ufundishaji.
Hivyo kitendo cha kuwaita hao wachezaji ambao kocha aliyepita hakuwaita kama akina Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Salum Abubakar na Paul Godfrey ‘Boxer’ kinatoa ishara kwamba kocha Etienne anataka kuonyesha kuwa yeye kama ‘professional coach’ atawatumia vipi hao wachezaji.
Maana moja ya sifa kubwa za ‘professional coach’ ni kuweza kuwasimamia wachezaji. Sasa hao walionekana hawana nidhamu, labda anataka kuonyesha kuwa anaweza kuwabadilisha na kuwaimarisha nidhamu yao.
Lakini pia kujenga ‘unity’ (umoja) ili nao wajione wana haki ya kuchezea timu ya taifa. Kuhusu mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za AFCON mwaka 2021, kwanza niseme kuwa kikubwa kinacho ‘determine’ (kinachoamua) kufuzu au kutofuzu ni kiwango cha maandalizi.
Nini ‘awareness’ (utayari) wa nchi katika kuwania kufuzu fainali hizo.
Tupo kwenye kundi ambalo pia lina timu za Tunisia, Libya na Guinea ya Ikweta. Kikubwa na cha msingi ambacho kinapaswa kufanyika ni kuangalia tulifanya nini kwenye fainali za AFCON zilizopita. Tathmini hiyo ndio itakuwa dira yetu. Lakini kingine ni ‘level of preparation’ (kiwango cha maandalizi). Wote tunafahamu kwamba Mataifa ya Kaskazini wamefanya uwekezaji mkubwa katika soka, lakini Guinea ya Ikweta ni taifa dogo ila litajipanga. Kikubwa ni kuanza kujiandaa kwa sababu mwaka 2021 sio mbali.