Yanga yaomba kucheza na Warundi Aigle Noir FC

Muktasari:

Yanga inaendelea na mazoezi Morogoro tayari kwa msimu mpya wa ligi ikiwa ni sambamba na mchezo wao wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya AS Vita.

Dar es Salaam.BAADA ya kuhairishwa kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Dodoma FC uongozi wa klabu ya Yanga upo katika mchakato wa kuomba mchezo wa kirafiki dhidi ya Aigle Noir FC ya nchini Burundi.

Timu hiyo kutoka Burundi ipo nchini kwaajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi inafanya mazoezi yake katika uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Mratibu wa klabu ya Yanga, Hafidh Saleh alisema mchezo wao dhidi ya Dodoma FC umehairishwa baada ya uongozi wa timu pinzani kuweka wazi kuwa hawajajiandaa kwaajili ya michezo ya kirafiki kwani timu ilikuwa bado haijakamilika.

"Uongozi wa Dodoma FC umesema umekamilisha usajili hivi karibuni na timu bado haijaingia kambini hivyo hawataweza kucheza na sisi kwasababu bado hawajafanya maandalizi yoyote na wanampango wa kuingia kambini Agosti Mosi mwaka huu,"

"Baada ya kuhairishwa kwa mchezo huo kabla hatujakutana na AS Vita tunaweza tukawa na mchezo mwingine wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu hiyo kinachosubiriwa ni ghalama za kuitoa Dar es Salaam na kuileta Morogoro ili tuweze kucheza nao lakini kila kitu kimekamilika," alisema Hafidh.