UKWELI NDIVYO ULIVYO: Kina Balinya, Deo Kanda, jueni mapema kazi mnayo

NGARAMBE ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 zimefikia tamati usiku wa kuamkia jana Jumamosi kwa Afrika kupata Bingwa Mpya wa michuano hiyo.

Algeria wamelibeba taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya kulisotea kwa miaka 29 tangu walipotwaa mara ya kwanza mwaka 1990 michuano hiyo ilipofanyikia katika ardhi yao, kwa kuifunga bao 1-0 Senegal ambao wameendelea gundu la mwaka 2002 walipofika fainali na kupiteza dhidi ya Cameroon.

Tanzania kama ilivyo kawaida, mashabiki wao wanajifariji baada ya kubaini walipangwa kundi moja na mabingwa wa michuano hiyo, kwani Algeria na Senegal walipangwa Kundi C sambamba na Taifa Stars na Harambee Stars ya Kenya.

Watanzania wanaona hakukuwa na haja ya Kocha Emmanuel Amunike kutimuliwa Stars kwa vile ilikuwa ngumu kwa kikosi cha Tanzania kuweza kutamba mbele ya wana fainali hao.

Wakati michuano hiyo ikifikia tamati kwa Algeria kuvuka boda la Misri kwa shangwe kwenda kwao na taji hilo baada ya kulisaka kwa muda mrefu, kazi ndio kwanza inaanza kwa Tanzania katika kusaka tiketi ya fainali za mwaka 2021.

Ndio, droo ya makundi ya michuano hiyo ijayo itakayofanyikia Cameroon, imepangwa na Stars kuangukia Kundi J na vigogo Tunisia, Libya na Guinea ya Ikweta katika kusaka tiketi ya kwenda kwa mara ya tatu kwenye fainali hizo za Afrika zitakazokuwa za 33.

Lakini wakati tukisubiri kuona Tanzania isiyo na Emmanuel Amunike itafanya nini katika mbio za kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2020 na hizo za Afcon 2021, mitaani kwa sasa ni tambo za mashabiki wa klabu za Simba na Yanga.

Kila mmoja anatambia nyota waliosajiliwa kwenye vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine ya ndani na ile ya kimataifa itayotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Timu hizo kwa pambano zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam na KMC zitaiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya Shirikisho la Soka (CAF) kuiongezea nafasi Tanzania katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu.

Kule Jangwani wameanza tambo baada ya timu yao kupata ushindi wa pili mfululizo ikianza kuibugiza Tanzanite Academy kwa mabao 11-1 na juzi kuicharaza Moro Kids kwa mabao 2-0.

Kelele zote zipo kwa nyota wao wa kufumania nyavu, Juma Balinya, Maybin Kalengo na Issa Bigirimana, mbali na Patrick Sibomana na Sadney Urikhob.

Wanaamini vijana hao wapya wataibeba Yanga maradufu na ilivyokuwa msimu uliopita ikiwategemea, Heritier Makambo, Amissi Tambwe na Ibrahim Ajibu ambao wote hawapo kwa sasa.

Upande wa pili kule, Simba wanatambia Wabrazili wao na nyota wengine wapya waliotua Msimbazi akiwamo Msudan Shiboub Sharraf Eldin, Deo Kanda na Ajibu aliyerejea nyumbani na wengine.

Simba na Yanga zinafahamika. Wepesi sana wa kusifia nyota wao na vilevile ni vigeugeu wa kuwachenjia nyota hao hao.

Kwa sasa mashabiki hao na wengine wa soka wana hamu ya kuwashuhudia nyota hao wapya wa klabu hizo katika Ligi Kuu Bara itakayoanza Agosti 23.

Wanataka kupima upepo kuona kama kina Makambo, Tambwe ama Emmanuel Okwi wameacha pengo kwenye klabu hizo ama la!

Makambo na Tambwe wameondoka Yanga wakiwa wamefunga jumla ya mabao 25 ikiwa ni karibu nusu ya mabao yote yaliyofungwa na Yanga msimu uliopita, hivyo kina Balinya, Kalengo na wenzao watakuwa na kazi ya kuthibitisha kuwa nao wamo.

Kasi walioanza nayo kwenye mechi za kutesti mitambo itapaswa kuendelezwa hata pale Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa itakavyoanza, vinginevyo wajiandae tu kusutwa.

Kuanzia vijiweni, mitaani mpaka kwenye mitandao ya kijamii, majina ya nyota hao yamekuwa wakijadiliwa na kuelezwa juu ya umahiri wao walionao katika kufumania nyavu, huku wengine wakiponda kuzifunga timu za Akademi ni sawa na kunoa kisu na kupina kwa kukatia mgomba.

Wale wa Simba wakiwapamba nyota wao waliopo kambini Afrika Kusini, wakiamini wakirejea wataiva na kuendeleza moto wa Msimbazi kama kawa.

Wengi wa mashabiki hao wanataka kuona nyota hao wakiifanya kazi iliyowaleta katika klabu hiyo kwa ufanisi kwenye mechi za ushindani, nami kwa kifupi tu, niwakaribishe tu kwa kuwaambia ‘karibuni Tanzania’, ila nikiwataka wawe makini ili kazi zao ziwe nyepesi.

Inawezekana ni kweli ni nyota hao wana vipaji vikubwa cha soka, ni kweli wameanza kuwakuna kila shabiki wa timu hizo na hata kutetemesha wale wa timu pinzani, ila kama watalewa sifa mapema huenda wakakwama kufanikisha yaliyotarajiwa kutoka kwao.

Soka la Tanzania lina mambo mengi, wanaowashangilia na kuwasifia leo ndio ambao watakaokuja kuwaponda na kuwatukana mbele ya safari. Kama hawaamini wajaribu kumpigia simu ama wamtafute Dan Sserunkuma, Steve Bengo kama sio Robert Ssentongo wawadokeze kilichowakuta Tanzania walipotua na kupokelewa kwa mbwembwe nyingi na mashabiki wa klabu hizo.

Kama hao itakuwa vigumu kwao kuwapata hao, basi mcheki hata Paul Kiongera na Simon Sserunkuma wakuwaleza walichokumbana nacho nchini.

Sitaki kuwakatisha tamaa, lakini nawakumbusha kuwa wamekuja Tanzania kucheza soka, hivyo wakomalie soka na kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa ufanisi kama alivyofanya Meddie Kagere, Tambwe, Chama ama Makamb... Wakikubali kupelekeshwa na kulewa sifa unazomwagiwa kisha wakajisahau, basi wajue mapema wameumia.

Wakiacha soka na kufuata starehe ambako huku zimejaa tele, walahi hawatakuwa na muda mrefu Jangwani ama kule Msimbazi. Watarudi kwao kwa aibu kubwa kama ilivyowahi kumkuta Laudit Mavugo.

Kwa bahati mbaya kama watavurunda mapema, wasitarajie watasindikizwa kwa bashasha kama ulivyopokewa, Simba na Yanga zimewapokea kwa shangwe kwa vile wanataka muwape burudani na kuwang’arisha katika Ligi Kuu na michuano ya Afrika.

Msipofanya hivyo hawatajali majina yenu, wala vipaji vyenu cha kucheza soka na hasa kufumania nyavu. Wamuulize Hamis Kiiza kilichomkuta alipokuwa Yanga na baadaye Simba alipoweza kufunga mabao 19 na kuwa Mfungaji Bora wa Simba misimu michache iliyopita, lakini kilichomkuta kwa kutemwa kikosini kimagumashi kama Tambwe.

Nawakumbusha tu, hapa ndio Bongo na watu wake, kubwa ni kuwakaribisha tena. Karibuni sana bandugu mfanye yenu.