Mtihani mkubwa Taifa Stars kufuzu AFCON 2021

Muktasari:

Tanzania kwa sasa iko chini ya kocha wa muda, Ettienne Ndayiragije baada ya Shirikisho la Soka (TFF) kumtimua kocha Mnigeria Emmanuel Amunike.

Dar es Salaam. Maandalizi ya mapema ya Taifa Stars ikiwa ni pamoja na kutafuta kocha mpya haraka ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuwa ni muhimu kwa timu yetu ya taifa ya soka baada ya droo ya kufuzu kwa fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2021 kuiweka Tanzania katika kundi gumu.
Tanzania ambayo iliondolewa katika hatua ya makundi ikiwa haina pointi hata moja katika fainali za AFCON zilizomalizika jana usiku huko Misri, imeangukia katika Kundi J lenye timu za Tunisia, Libya na Guinea ya Ikweta katika kuwania kufuzu kwa fainali zijazo 2021 zitakazofanyika nchini Cameroon.
Stars itakuwa na kazi ya ziada kuvuka viunzi na kufuzu dhidi ya mataifa ambayo yametuzidi viwango vya ubora wa soka duniani vinavyotolewa na FIFA  -- Tunisia inayoshika nafasi ya 25 duniani na ya pili Afrika nyuma ya Senegal na ambayo ilitolewa katika nusu-fainali ya AFCON ya mwaka huu, na Libya inayoshika nafasi ya 105 duniani. Tanzania ni ya 131 na imeipita Guinea ya Ikweta pekee inayoshika nafasi ya 141 duniani.
Tanzania kwa sasa iko chini ya kocha wa muda, Ettienne Ndayiragije baada ya Shirikisho la Soka (TFF) kumtimua kocha Mnigeria Emmanuel Amunike.
Droo ya juzi usiku iliyochezeshwa jijini Cairo ilipanga makundi 12 ya timu nne kila moja, ambapo timu mbili za juu zitafuzu kwenda AFCON 2021.
Mchambuzi wa mpira wa miguu, Mwalimu Alex Kashasha alisema hakuna muda wa kusubiri baada ya makundi hayo kupangwa na badala yake maandalizi yanapaswa kupangwa sasa.
“Kuhusu mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za AFCON mwaka 2021, kwanza niseme kuwa kikubwa kinacho ‘determine’ (kinachoamua) kufuzu au kutofuzu ni kiwango cha maandalizi. Na ‘awareness’ (utayari) wa nchi katika kuwania kufuzu fainali hizo.
“Pia ‘level of preparation’ (kiwango cha maandalizi). Wote tunafahamu kwamba Mataifa ya Kaskazini wamefanya ‘investment’ (uwekezaji) wa kutosha kwenye mpira wa miguu lakini Guinea ya Ikweta ni taifa dogo lakini bila shaka litajiandaa vizuri.
“Kikubwa ni kwamba muda umeshaisha na huu ni wakati wa kuanza kujiandaa kwa sababu mwaka 2021 sio mbali,” alisema Kashasha.
Kocha msaidizi wa muda wa Taifa Stars, Seleman Matola alisema sio kundi tishio kwa timu hiyo na inaweza kufanya vizuri.
“Makundi nimeyaona na nimeridhika na kundi ambalo tumepangwa tukiwa pamoja na timu za Tunisia, Guinea ya Ikweta na Libya.
“Sio kundi gumu kwetu ikiwa tutajipanga vizuri kwani hizo timu zinafungika. Kikubwa ni kufanya maandalizi ya uhakika. Ni timu nzuri ambazo tumepangwa nazo lakini tukijiandaa vizuri tutapata matokeo mazuri dhidi yao,” alisema Matola.
Beki za zamani wa Stars, Boniface Pawasa alitilia mkazo suala la maandalizi na kudai kuwa ndio silaha ya kufanikiwa.
“Siku hizi hakuna timu kubwa wala ndogo. Ile inayojiandaa vizuri ndio inapata matokeo hivyo kama tutachanga vyema karata zetu, naona tuna nafasi ya kufuzu,” alisema Pawasa.