Mshindi wa bodaboda ya Mwanaspoti akabidhiwa

Muktasari:

Mshindi wa mwisho kutoka Magomeni jijini hapa Wilfred Magige alijishindia kitita cha Sh 100,000, alielezea pesa hiyo itakuwa kama msingi kwake kwani atakwenda kununua magazeti ya Mwanaspoti yote ili kupata zawadi ya bodaboda kwani hayo ndio malengo yake.

MSHINDI wa shindano la shida mchongo na Mwanaspoti aliyepata zawadi ya pikipiki (bodaboda), Giziraly Malibiche mkazi wa Tandika jijini Dar es Salaam, amekabidhiwa zawadi yake leo Alhamisi na kueleza kuwa zawadi hiyo ataitumia kama kitega uchumi chake.
Malibiche amesema wakati anapigiwa simu na kupewa taarifa ya ushindi huo alikuwa na mke wake jambo ambalo alishindwa kuamini na hata kushindwa kula chakula alichoandaliwa.
"Bodaboda hii itakuwa kitega uchumi changu kwa kuitumia kama chombo cha usafiri ambacho kitakuwa kinabeba abiria kisha baada ya muda nitakuwa napata kipato uzuri wake mwenyewe naweza kuendesha au nikiamua nitafanya maamuzi ya kumpa ajira kijana mwenzangu,"
"Mwanaspoti imebadilisha maisha yangu mara baada ya kunipa zawadi hii ambayo itakuwa inanipatia kipato mbali ya kazi yangu ya ulinzi ninayoifanya, niwaombe na kuwasisitiza  Watanzania wote kununua na kucheza shindano hili kwani ni la kweli," anasema Malibiche.
Katika hatua nyingine washindi wawili Daud Charles mkazi wa Mbezi Magoe alikabidhiwa zawadi yake ya simu ya mkononi ya kisasa (Smartphone), na kueleza itakwenda kumsaidia katika mambo mengi.
"Sikuwa na smartphone kwa muda mrefu lakini baada ya kupata katika shindano hili la shinda mchongo wa Mwanaspoti umenipatia simu ambayo nitakuwa nafuatilia habari na mambo ambayo yanaendelea katika mitandao ya kijamii lakini hata kuwasiliana na ndugu zangu," alisema Charles.
Mshindi wa mwisho kutoka Magomeni jijini hapa Wilfred Magige alijishindia kitita cha Sh 100,000, alielezea pesa hiyo itakuwa kama msingi kwake kwani atakwenda kununua magazeti ya Mwanaspoti yote ili kupata zawadi ya bodaboda kwani hayo ndio malengo yake.
"Niliwai kushinda bodaboda, Luninga na smartphone katika shindano ya Mwanaspoti 2007, na mwaka huu nimeshinda Sh 100,000 inakuwa zawadi yangu ya pili lakini malengo yangu ni kupata bodaboda, hivyo hii pesa nitakwenda kununua mageziti ya Mwanaspoti na nitajaza ili kushinda tena," alisema Magige.