Waendesha baiskeli watambiana Tamasha la Majimaji Selebuka

Muktasari:

Tamasha la Majimaji Selebuka limeingia msimu wa tano mwaka huu huandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Songea Mississippi (So-Mi), linatarajiwa kufikia tamati kesho Jumamosi.

Dar es Salaam. Waendesha baiskeli waliotikisa katika mbio za Tamasha la Majimaji Selebuka mwaka jana kila mmoja akijinasibu kutwaa ubingwa huo tena mwaka katika shindano litakalofanyika Jumamosi hii mjini Songea.

Mbio hizo za Kilomita 100 zitaanzia kwenye Viwanja vya Makumbusho ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na kwenda kugeuzia eneo la Liganga kisha kurejea kwenye viwanja hivyo zikiwa na lengo la kuhimiza mazoezi kwa afya.

Tayari bingwa wa Taifa mbio za Baiskeli, Masunda Duba kutoka Simiyu na mwenzake Boniphace Masunda wameishawasili huku wakali wengine kutoka Arusha, Manyara, Mbeya, Iringa na wenyeji Ruvuma wakitarajiwa kuwasili mjini Songea wakati wowote.

Akizungumza mara baada kuwasili, Duba alisema amejiandaa vema na ni matarajio yake kuibuka mshindi japokuwa si mbio za ushindani lakini anahitaji heshima.

"Lengo ni kuhakikisha natetea nafasi yangu. Mwaka jana ilikuwa mara yangu ya kwanza kushiriki mbio za Majimaji Selebuka hivyo changamoto zilikuwa nyingi, tofauti na sasa nalijua vizuri tamasha hili kubwa Kusini mwa Tanzania,” alisema Duba.

Msimu uliopita Duba aligeuka gumzo mbali na kutumia muda mfupi zaidi, saa 2:53.05 bali kushiriki bila vifaa vya michezo kama kofia ngumu, bila viatu huku akitumia baiskeli ya kawaida iliyopachikwa jina la ‘ya kwendea shambani’.

Boniphace Masunda ambaye msimu uliopita alikuwa wa pili akitumia saa 2:54.21 alisema yuko vizuri na amekuja kuweka rekodi ya kumtoa Duba kwenye reli ya ubingwa.

Mratibu wa Tamasha la Majimaji Selebuka, Reinfrida Lwezaura alisema tamasha hilo limefanikiwa kurejesha msisimko katika mbio za baiskeli tangu kuanzishwa kwake.

Lwezaura alisema mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake ataibuka na kitita cha Sh1Milioni, wa pili 700,000 wa tatu 500,000 huku wa nne hadi kumi wakijipoza na Sh 50,000 kila mmoja.