Christian Bella kupamba shindano la Miss Manyara

Muktasari:

Zawadi kwa mshindi ni Sh1.5 milioni, mshindi wa pili atapata Sh1 milioni huku wa tatu ataondoka na Sh500,000 wakati kuanzia mshiriki wa nne hadi 16 kila mmoja atapewa Sh100,000 kifuta jasho

ARUSHA. Jumla ya warembo 16 kutoka mkoani Manyara wanatarajia kupanda jukwaani kesho Jumaa usiku mjini Babati kuwania taji la Miss Manyara huku mwanamuziki wa muziki wa dansi, Christian Bella akitarajiwa kutoa burudani.

Shindano hilo linatarajia kufanyika ukumbi wa The Champions Lounge Babati mjini, ambapo washindi watatu watashiriki shindano la kumsaka Miss Tanzania Kanda ya Kaskazini litakalofanyika Julai 25 mwaka huu jijini Arusha.

Mratibu wa shindano hilo, Akon Clement amesema maandalizi yamekamilika ambapo kiingilio ni Sh 10,000 kawaida na Sh 20,000 VIP na kuongeza kuwa shindano la mwaka huu litakuwa na ushindani mkubwa kwani kila mrembo anaonekana kuwa na uwezo wa hali ya juu.

Alisema kabla ya mchujo walikuwa warembo 21 ambapo walitumia kigezo cha umri, mvuto, uwezo wa kujitambua ili kuwapata hao 16.

Akon alisema warembo hao wakiwa kambini walitafutiwa wataalam wa fani na taaluma mbalimbali ambao walikuwa wanawafundisha kuhusiana na stadi za maisha kwani wanaamini kupitia warembo hao mkoa wa Manyara itatangazika vyema.

Shindano hilo linadhaminiwa na kampuni mbalimbali ambapo zawadi kwa mshindi ni Sh 1.5 milioni, mshindi wa pili atapata Sh 1 milioni huku wa tatu ataondoka na Sh 500,000 wakati kuanzia mshiriki wa nne hadi 16 kila mmoja atapewa Sh100,000 kama kifuta jasho.