Huku Manula na Beno kule Tshabalala, Gadiel patachimbika

Muktasari:

Simba imefanya usajili wa wachezaji wengi bora kwa lengo la kujenga kikosi chake kuhakikisha wanatetea ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kufanya vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa

Dar es Salaam. Wachezaji wapya wa Simba, kipa Benno Kakolanya na beki Gadiel Michael wamesema wapo tayari kwa ushindani kutoka kwa Aish Manula na Mohammed Hussein 'Tshabalala'.

Simba imewasajili Kakolanya na Gadiel wakitokea Yanga, lakini wawili hao wanategemea kupata ushindani mkubwa kutoka kwa Manula na Tshabalala waliokuwa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara.

Ushindani utakuwa beki wa kushoto Gadiel na Tshabalala si katika kikosi cha Simba mbali hata katika timu ya Taifa 'Taifa Stars' ambapo huku Gidiel amekuwa akipata nafasi zaidi.

Vita nyingine itakuwa nafasi ya kipa Manula na Kakolanya ushindani wao ulianza katika kikosi cha Taifa Stars ingawa Manula alikuwa anacheza mara kwa mara.

Kakolanya alifunguka kuwa mpaka amemua kufanya uamuzi ya kujiunga na Simba basi alitambua kuwa anakwenda kukutana na changamoto ya kuwania namba katika timu wenye kipa mzoefu.

"Manula ni kipa mzoefu alianza kucheza kuliko mimi, lakini amecheza kwa muda mrefu mpaka katika ngazi ya juu kwa maana ya timu ya Taifa kwahiyo ni kazi kubwa ya kushindana nae hilo nalitambua, lakini nitakuwa nachukua ujuzi na kujifunza kutoka kwake," alisema Kakolanya.

Naye Gadiel alisema ushindani wa kuwania nafasi ya kucheza upo katika timu yoyote ile ambayo angekwenda kucheza kwa maana hiyo kukutana na ushindani dhidi ya Tshabalala wala hana shida nalo na yupo tayari kwa mapambano.

"Kikubwa nitakuwa natimiza majukumu yangu ambayo nitakuwa napangiwa na makocha wote na mwisho wa siku wao ndio wenye jukumu la kuamua yule wa kumpa nafasi ya kucheza," alisema Gadiel.