TFF na Mwakyembe: Kimbunga kwenye kikombe cha chai?

Muktasari:

Labda swali la kujiuliza ni kwanini walimu huwa wanafukuzwa? Kuna sababu moja maalumu ya kufukuza kocha? Ukweli hakuna sababu moja pekee inayoweza kutumiwa kufukuza kocha. Tuangalie kwa wenzetu walioendelea kujua ni mambo yapi yanaweza kumfukuza kocha.

WAINGEREZA wana msemo; A storm in a tea cup ambao tafsiri yake kwa Lugha ya Kiswahili ni kimbunga ndani ya kikombe. Huu ni wa kisasa lakini ulitanguliwa na msemo mwingine wa zamani uliosema Much ado for nothing. Tafsiri ni ileile kwa Kiswahili na maana ni moja.
Maana yake ni watu kufanya tatizo lionekane kubwa wakati jambo lenyewe ni dogo kabisa. Yaani kimbunga cha kwenye kikombe cha chai kinaweza kumuua nani? Kinaanzia na kuishia humohumo kwenye kikombe. Hamna kitu. Wakati mwingine ikimaanisha watu kuleta mgogoro usio na maana yoyote.
Nimekuwa nasoma magazeti ya Tanzania na mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu kinachoendelea baada ya Taifa Stars kuondoshwa katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yanayoendelea Misri. Nitaangaza machache na kuonyesha karibu kila kitu ni cha kawaida na hakuna mgogoro au tatizo linalotakiwa kuzuka.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wiki iliyopita lilitangaza kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike. Unaweza kuwa uamuzi sahihi au si sahihi kwa baadhi ya watu, lakini suala la kuachana na makocha ni la kawaida katika mchezo wa mpira.
Labda swali la kujiuliza ni kwanini walimu huwa wanafukuzwa? Kuna sababu moja maalumu ya kufukuza kocha? Ukweli hakuna sababu moja pekee inayoweza kutumiwa kufukuza kocha. Tuangalie kwa wenzetu walioendelea kujua ni mambo yapi yanaweza kumfukuza kocha.
Sababu ya kwanza ni matokeo mabaya. Hakuna timu ambayo inapenda kupata matokeo mabaya katika ulimwengu huu, ambapo soka ni mojawapo ya biashara kubwa za matokeo uwanjani ni mojawapo ya vivutio kwa matajiri na wawekezaji.
Manchester United ilimuajiri David Moyes kwa mkataba mrefu lakini ikamfukuza baada ya kuona matokeo yanakuwa mabaya. Hata Misri imemfukuza aliyekuwa kocha wake. Javier Agguirre kwa sababu ya kutolewa katika mashindano ya mwaka huu ambayo wengi walikuwa wakiipa Misri kutwaa kombe.
Simba iliwahi kuachana na Moses Basena wakati ikiwa inaongoza ligi kwa sababu tu staili yake ya uchezaji haikuwa inaendana na falsafa ya klabu. Real Madrid ilimfukuza kazi Fabio Capello baada ya klabu hiyo kutwaa ubingwa kwa maelezo, timu ilikuwa haivutii ikicheza.
Juventus imeachana na Massimilliano Allegri kwa sababu uongozi umeona ingawa ametwaa ubingwa wa Italia mara sita mfululizo, hawezi kuwapa tena zaidi ya anachoweza kuwapa.
Jose Mourinho alifukuzwa Madrid kwa sababu ya kutokuwa na maelewano na nyota wa klabu hiyo ingawa alikuwa akifanya vizuri tu. Rafael Benitez ameachana na Newcastle kwa sababu ya maelewano mabovu na mmiliki wa klabu hiyo, Mike Ashley. Kwa hiyo kuna sababu zaidi ya moja za mwajiri kuachana na kocha.
Kwa sababu sisi hatuko ndani ya TFF, hatuwezi kujua ni sababu ipi hasa ambayo imesababisha Amunike aondolewe miongoni mwa sababu nyingi zinazoweza kuwapo. Nilidhani badala ya kwenda mbali na kuwaambia viongozi wa TFF nao wawajibike, tunaweza kukaa chini na kukubaliana ni aina gani ya kocha anafaa kuajiriwa na Tanzania kwa sasa.
Kama ningeulizwa, ningesema kuna vigezo kama vitano ambavyo vinatakiwa kuangaliwa kwenye kutafuta kocha mpya. Mosi, ni muhimu awe na rekodi ya kutwaa makombe huko alikokuwa, awe na tabia ya kukaa katika timu au nchi husika kwa muda mrefu (sio kocha ambaye anajulikana anakaa mwaka mmoja au miwili tu halafu anaondoka), awe na uzoefu wa soka la Afrika, awe na uthubutu wa kufanya maamuzi pasipo kuingiliwa na mwenye mtandao wa marafiki katika klabu za nje.
Hili la mwisho ni la muhimu katika soka la kisasa kwa sababu Tanzania inahitaji kuwa na wachezaji wengi zaidi nje ya nchi; hususan katika nchi zilizoendelea kisoka ili kutengeneza timu ya wachezaji wanaojua nini kinahitajika wakiwa ndani ya uwanja na wenye uelewa wa kutosha wa kimbinu.
Haya ndiyo mambo ambayo watu wanatakiwa kujadiliana na kupanga ili nchi yetu isonge mbele kisoka. Jambo la kocha kama Amunike kuondolewa kwenye timu halitakiwi kuwa zito sana kiasi cha kutoa picha ya mgogoro mkubwa.
Ni bahati mbaya habari hizi za Mwakyembe na TFF zimeinyima nafasi jamii ya Watanzania kujadili na kufahamu maana ya hatua ya shirikisho kuingia mkataba na shule ya Fountain ya Dodoma kwenye kutoa elimu kwa watoto wa Tanzania wenye vipaji vya soka.
Kwangu, hizi zilikuwa habari za kusisimua zaidi kwa wiki hii. Kwa mara ya kwanza, taifa letu limetengeneza mpango wa kuwaandaa kitaaluma na kimichezo watoto wenye umri mdogo kwa ajili ya kuja kuwatumia baadaye.
Katika umri wangu huu, nimeshuhudia vijana wa Kitanzania waliokuwa na uwezo mzuri wa kisoka wakiachana na mchezo huo na kufanya shughuli nyingine. Kuna wengine sasa hivi ni madereva wa bodaboda huku wengine wakiuza mitumba.
Uzuri wa elimu ya darasani kwa watoto ni kwamba inawapa uelewa mpana wa mambo ya dunia. Unawapa uwezo wa kuzungumza walau lugha moja ya kimataifa na kuwajengea msingi wa kuweza kufundishika. Kumfundisha mbinu za soka mchezaji, ambaye hajawahi kupita darasani ni jambo gumu na hili limekuwa ni mojawapo ya matatizo yasiyosemwa ya soka letu.
Faida nyingine mtoto aliyepata elimu nzuri, ataweza kupata fursa ya kufanya kazi yenye utu endapo ndoto zake za kucheza soka hazitatimia. Pasipo shule, mchezaji aliyeshindwa walau kutokana na majeraha tu, anaweza kuibuka kuja kuwa muathirika wa madawa ya kulevya au kufanya vitendo visivyokubalika kisheria.
Mpango kama huu unaweza usiwe na faida katika miaka mitano ijayo, lakini tunaweza kuvuna matunda yake pengine kuanzia miaka kumi ijayo. Hii ndiyo mipango ya kisoka ambayo pengine wengi wetu tunatakiwa kuitia moyo na kuiombea uendelevu.
Maneno ya Mwakyembe yalinirudisha nyuma sana kuhusu uhusiano baina ya serikali na TFF. Ukiniuliza, nadhani uhusiano baina ya vyombo hivyo viwili umekuwa mzuri sana katika miaka hii kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
Huko nyuma, nikirejea nyakati za kina Muhidin Ndolanga, hali ilikuwa tete sana. Siku hizi ni kawaida kuona Mwakyembe akinywa chai na Rais wa TFF, Wallace Karia.