Singano aula TP Mazembe

Thursday July 11 2019

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Mshambuliaji Ramadhan Singano 'Mesi' amesaini mkataba wa miaka minne kuitumikia TP Mazembe.

 

Singano mesaini mkataba huo baada ya kuachwa huru na Azam FC na atakuwa sehemu ya wachezaji wa kikosi hicho msimu ujao akiungana na Mtanzania Mwingine Eliud Ambokile.

 

Mshambuliaji huyo aliondoka nchini juzi Jumanne kwa ndege ya Shirika la Kenya akipitia Nairobi.

 

Amesaini jioni ya leo Alhamisi ndani ya ofisi ya tajiri wa DR Congo, Moise Katumbi iliyopo Lubumbashi.

 

Safari ya Singano ilikuwa pamoja na Mrisho Ngassa lakini yeye dili lake liligoma baada ya kusajiliwa na Yanga. Yanga waliposikia safari, wakamwekea pesa mezani akasaini.

 

Pia, awali alikuwa asajiliwe Ibrahim Ajibu ambaye alikataa na kujiunga na Simba akitokea Yanga.

 

Singano anakuwa mchezaji wa pili Mtanzania kusajiliwa na TP Mazembe msimu huu baada ya Ambokile.

 

Awali wachezaji, Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu wa JS Saoura ya Algeria walicheza hapo.

Advertisement