Azam FC yafagilia Kagame Cup kuwajenga kimataifa

Muktasari:

Azam ndio bingwa mtetezi wa mashindano ya Kagame Cup ikiwa imetwaa ubingwa huo mara mbili mfululizo, mwaka 2015 na 2018 huku bingwa wa kihistoria akiwa ni Simba aliyetwaa mara sita

Dar es Salaam. Wakati ikijiandaa kurusha kete yake ya mwisho kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) leo dhidi ya Bandari FC, Azam FC imetamba kuwa mashindano hayo yamekuwa na faida kubwa kwao.

Azam inayoshika nafasi ya pili kwenye kundi B inahitajika kupata ushindi kwenye mechi hiyo ili ikate tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali vinginevyo itajiweka kwenye mazingira magumu ya kutetea ubingwa wa mashindano hayo kwani inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu nyuma ya KCCA yenye pointi nne.

Kocha msaidizi wa Azam FC, Iddi Cheche alisema kuwa mashindano hayo yamekuja katika wakati muafaka kwao, wakijiandaa pia kwa ajili ya msimu ujao.

"Unajua sasa hivi ni wakati wa msimu wa maandalizi. Tuna maingizo mapya na tuna wachezaji vijana wamechanganyika kwa hiyo tunapoanza hali hiyo inakuwa inasumbua kidogo.

Lakini ni kazi yetu kurekebisha mambo haya na kuhakikisha tunafanya lile lililotuleta huku kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu. Nafikiri tumepata nafasi ya kutosha na vijana wameelewa nini tumewaelekeza na watatuletea matunda.

Ni mashindano makubwa nambayo yanakupa changamoto mwalimu na mchezaji vilevile kwa sababu unapokuwa unacheza na mtu kutoka nchi tofauti kuna kitu kingine tofauti unakipata," alisema Cheche.

Kuhusu mechi ya kesho alisema wamejiandaa kuhakikisha wanapata ushindi.

"Yote kwa yote sisi tunasema tunangoja siku ya kesho muda ufike tufanye kile tulichojiandaa nacho. Ili tuwaonyeshe Watanzania na Wanayarwanda huku kuwa sisi tuna nini kama Mabingwa watetezi," alitamba Cheche