Azam yapokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa KCCA

Muktasari:

Azam ni bingwa mara mbili wa Kombe la Kagame na mwaka huu inajipanga kutetea taji hilo nchini Rwanda.

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa kombe la Kagame, Azam wamekumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa KCCA ya Uganda.

Awali Azam ilianza kampeni za kutetea ubingwa huo nchini Rwanda, Julai 7 kwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mukura.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa wa pili kwa timu zote mbili, Azam iliruhusu bao hilo, dakika ya 43, walilofungwa na Anaku Sadat.

Kipigo ilichopata Azam ni cha kwanza kwa kocha, Etienne Ndayiragije tangu akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo.

Kikosi kamili cha Azam kilichoanza katika mchezo uwanja wa Huye  huo ni  Razak Abalora, Gadafi Said, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Yakubu Mohammed, Salmin Hoza, Idd Kipagwile, Abdallah Masoud, Donald Ngoma,  Abalkasim Khamis na Idd Seleman.

Azam wamesaliwa na mchezo mmoja katika kundi B ambao watacheza, Ijumaa na Bandari Kenya.