Miraji: Usajili wa Gadiel ni funga kazi Simba

Muktasari:

Uwezo wa mchezaji unafanyika kuwa muhimu ndani ya timu anayoichezea, kitendo cha aliyekuwa beki wa Yanga, Gadiel Michael kusaini Simba imeonekana kuwa bahati ndani ya klabu yake mpya.

Dar es Salaam. Winga mpya wa Simba, Miraji Athuman amesema kitendo cha mabingwa hao kumnasa beki namba mbili, Gadiel Michael anaona wamepata jembe la maana.

Miraji hakuficha furaha yake ya kukutana na Gadiel Simba kwamba anapenda kucheza na wachezaji ambao wanacheza nafasi zaidi ya moja kwamba wanatoa changamoto kwa wengine.

Katika vitu alivyovitaja alivyomuona navyo Gadiel ni jinsi ambavyo anakaba na kushambulia kila anapopata nafasi , jambo alilodai linakuwa linawasumbua wapinzani.

"Ukiwa na mchezaji ambaye unaweza ukamkuta kila sehemu uwanjani huyu anapaswa kuheshimiwa sana kwani anakuwa na mazoezi ya kutosha na pumzi.

"Lakini pia ndio uchezaji wa kisasa ili mchezaji, ufike mbali lazima ujue namna ya kujituma zaidi ya nafasi yako, hilo linakuwa linasaidia hata kuziba mapungufu ya mwingine,"anasema.

Simba imemsajili Athuman kutoka Lipuli ya Iringa kuwa mmoja wa wachezaji ambao wataongeza nguvu kwenye kikosi hicho kwa msimu ujao.