Real Madrid yapiga hesabu kali kumnasa Pogba

Muktasari:

Pogba amekuwa akitakiwa na klabu za Real Madrid na Juventus lakini hata hivyo alisafiri katika kikosi cha kocha, Ole Gunnar Solskjaer ingawa inaeleweka kwamba msimamo wake wa kutaka kuuza klabuni hapo upo pale pale.

MADRID, HISPANIA. Real Madrid ni wataalamu bwana wa kunasa wachezaji wakubwa. Wametumia janja ya nyani kuhakikisha wanainasa saini ya staa wa Manchester United, Paul Pogba. Hawataki shari na mtu wakati wanamtaka mtu wao.

Inaaminika kwamba wao ndio ambao wamemshauri staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa kuungana na wachezaji wenzake wa Manchester United katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya ambayo imeweka nchini Australia katika mji wa Perth.

Pogba amesafiri na wenzake kwenda Australia na kisha Mashariki ya mbali ingawa kulikuwa na wasiwasi kutoka kwa mabosi wa Real Madrid kwamba huenda staa huyo angegoma kwenda katika ziara hiyo baada ya wakala wake, Mino Raiola kujitokeza hadharani na kuthibitisha kwamba nyota huyo anataka kuondoka.

Pogba amekuwa akitakiwa na klabu za Real Madrid na Juventus lakini hata hivyo alisafiri katika kikosi cha kocha, Ole Gunnar Solskjaer ingawa inaeleweka kwamba msimamo wake wa kutaka kuuza klabuni hapo upo pale pale.

United wanaweza kulazimika staa huyo waliyemnunua kutoka Juventus kwa dau la pauni 89 milioni na kuvunja rekodi miaka mitatu iliyopita lakini wamepanga kumuuza kwa dau la pauni 160 milioni kama watalazimika kufanya hivyo.

Na sasa imejulikana kwamba Madrid ndio ambao walimwambia Pogba aende katika ziara hiyo na Manchester United kwa sababu hawataki ugomvi wowote na United kuelekea katika mazungumzo ya kumnunua staa huyo anayetakiwa na kocha, Zinedine Zidane ambaye ni Mfaransa mwenzake.

Pogba alikuwa miongoni mwa mastaa 28 wa United waliopaa kwenda mji wa Perth Jumapili kwa ajili ya maandalizi ya wiki mbili na nusu katika nchi za Australia na Mashariki ya mbali na kwa mujibu wa taarifa kutoka Hispania zinadai kwamba Madrid hawataki ugomvi na United katika suala hili.

Hofu yao inakuja kutokana na ukweli kwamba wao Madrid wanashindana na Juventus katika mbio za kumuwania Pogba na endapo watawaudhi United kuna uwezekano mkubwa United wakaamua kufanya biashara na Juventus.

Habari zaidi zinadaiwa kwamba Zidane anamuona Pogba, ambaye ni Mfaransa mwenzake, kama mchezaji muhimu katika kurudisha ubabe wa Madrid eneo la kiungo kuelekea katika ufalme wa mataji ya nyumbani na lile la ubingwa wa Ulaya.

Hata hivyo United wameendelea kung’ang’ania kwamba hawana mpango wa kumuuza staa huyo ingawa awali tayari Madrid walifanya umafia mwingine wa kumwambia Pogba aanzishe taarifa za kuomba kuondoka kikosini hapo.

Akiwa katika ziara ya promosheni ya kampuni ya Adidas jijini Tokyo nchini Japan hivi karibuni, staa huyo alikaririwa akiomba kuuzwa na wababe hao wa Old Trafford kitu ambacho kiliwashtua mabosi wa timu hiyo.

“Itakuwa muda mzuri wa kupata changamoto kwingine. Nafikiria kuhusu hilo. Nimekuwa Manchester kwa miaka mitatu na nimekuwa nikifanya vizuri. Nimekuwa na nyakati nzuri na nimekuwa na nyakati mbaya, kama mtu mwingine yeyote.” Alikaririwa Pogba nchini Japan.

 

Na mwishoni mwa wiki iliyopita, wakala wake, Mino Raiola naye aliongeza presha kwa kuthibitisha kwamba staa huyo anataka kuondoka OId Trafford na kila mtu anafahamu hilo.

“Kila mtu ndani ya klabu kuanzia Meneja hadi kocha anajua matamanio ya Paul. Kila mtu anafahamu nia ya Paul kuondoka zake. Tupo katika mchakato huo.” Alisema Wakala huyo.

Miongoni mwa mastaa waliopaa kwenda Australia ni pamoja na mshambuliaji wa kimataifa wa Ubelgiji, Romelu Lukaku ambaye naye amekuwa akihusishwa kwenda Inter Milan anakotakiwa kwa udi na uvumba.

Wengine waliondoka ni pamoja na mastaa wapya klabuni hapo, mlinzi Aaron Wan-Bissaka aliyenunuliwa kutoka Crystal Palace kwa dau la pauni 50 milioni pamoja na Daniel James aliyenunuliwa kutoka Swansea kwa dau la pauni 18 milioni.