Fenerbahce yajitosa kwa Ozil yajipanga kumng’oa Arsenal

Muktasari:

Ozil utoto mwake alikuwa akiishabikia Fenerbahce na timu hiyo inataka kumchukua huku ikisema italipa mshahara wa Pauni 8 milioni tu kwa mwaka kutoka Pauni 13.5 milioni

London, England. Fenerbahce imechungulia presha fursa na sasa inamtaka kumchukua supastaa Mesut Ozil baada ya kutambua kwamba Arsenal watachangulia kulipa asilimia fulani ya mshahara wake.

Taarifa za kutoka Uturuki zinadai kwamba klabu hiyo inataka kunasa huduma ya Ozil, ambaye maisha yake hayaonekani kuwa mazuri huko kwenye kikois cha Arsenal chini ya kocha Unai Emery. Msimu uliopita Mjerumani huyo alisugua sana benchi kwa sababu zilizoelezwa kuwa ni za kiufundi.

Huko kwenye kikosi cha Arsenal, Ozil ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi na sasa wanataka kumtoa kwa mkopo ili tu wapunguze bili yao ya mishahara, kitu ambacho Fenerbahce imeripotiwa imekubali kumchukua.

Ozil utoto mwake alikuwa akiishabikia Fenerbahce na timu hiyo inataka kumchukua huku ikisema italipa mshahara wa Pauni 8 milioni tu kwa mwaka kutoka Pauni 13.5 milioni, hivyo pesa nyingine zilizobaki watalipa Arsenal.

Kwa maana hiyo, Arsenal watakuwa wakilipa Pauni 5.5 milioni zilizobaki, kitu ambacho kitakuwa kimewapunguzia kwa namna fulani bajeti yao ya mishahara huko Emirates. Ozil mwenyewe anataka kubaki Arsenal, akidai kwamba anapenda maisha ya London.

Staa wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Petit amesema kwamba Ozil hata tena yale maajabu yake ya zamani, akisema: "Namheshimu sana Ozil lakini kwa sasa siyo yule niliyekuwa nikimtazama miaka michache iliyopita, kipindi alichokuwa mmoja wa viungo bora kabisa wa ushambuliaji duniani. Ilikuwa raha kumtazama.

"Sasa hivi, hakuna raha yoyote, wala huhitaji tena kumwona kwenye timu kwa sababu hana maajabu."