Kahata afichua mazito ya usajili wake Simba

Muktasari:

Kiungo huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto,  alisema kuwa Simba ilionyesha nia muda mrefu na hata alipokuwa Misri kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) maofisa wake waliendelea kumfuatilia  kwa karibu.

Dar es Salaam. Kiungo mpya wa kimataifa wa Simba, Francis Kahata amesema hakuwa na dhamira ya kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa mtandao wa Goal, Kahata alisema kitendo cha Gor Mahia ya Kenya kutothamini mchango wake ndani ya klabu hiyo kilimsukuma kuondoka.
Nyota huyo wa Harambee Stars, alisema endapo Gor Mahia ingempa ofa ya kuongeza mkataba angebaki Kenya.
Kahata alisema viongozi wa Gor Mahia hawakumfuata kuzungumza naye kuhusu mkataba wake hata ulipokuwa ukielekea ukingoni.
“Wakati mkataba wangu unakaribia kumalizika hakuna kiongozi wa Gor  Mahia aliyenifuata tuzungumze kwa ajili ya kuongeza. Nilisubiri, lakini hakuna aliyejitokeza.
“Sikupenda kuondoka lakini nimelazimika kuchukua uamuzi kwa kuwa tayari Simba walikuwa wakinifuatilia na walionyesha dhamira ya kunisajili,” alisema Kahata.
Kiungo huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto,  alisema kuwa Simba ilionyesha nia muda mrefu na hata alipokuwa Misri kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) maofisa wake waliendelea kumfuatilia  kwa karibu.
Kahata aliyedumu Gor Mahia kwa miaka mitatu na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya, ametia saini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Simba.