Lamata kama una mwonekano huu mfuate akupe dili

Muktasari:

Licha ya kuwa shabiki wa Yanga, Lamata anaweka wazi kwake yeye soka si kama mpira wa kikapu na hata ndani kwake ameweka picha ya mchezaji wa mchezo huo, Steve Kerr.

ACHANA na mambo ya misosi ambayo mwenyewe amesema ndo habari kwake, na hasa pilau. Uliona pia amekimbiwa na wanaume kwa sababu ya mapenzi yake kwenye masuala ya filamu. Hata hivyo, kuhusu mapenzi yake kwenye sanaa hiyo, ana watu wake buana. Msikie mwenyewe anavyoendelea kutiririka kuhusu maisha yake na kazi yake.

KUMBE ANAANGALIA SURA
Kuna watu wanazungumza na Lamata anawasikia, eti anapenda kufanya kazi na jamaa wenye mvuto au wasichana warembo na wale wa kawaida anawapotezea.
Lamata anafafanua maneno hayo na kusema ni kweli kabisa kwani kupenda mahendisam boi na wadada warembo mbali na vipaji walivyonavyo, wanaifanya filamu kuwa na mvuto.
“Kitu cha kwanza ambacho huwa naangalia ni kipaji lakini cha pili ni mwonekano wa mhusika ukiwa mzuri inakuwa poa zaidi. Pale mcheza filamu anapokuwa anavutia kuna mvuto fulani kwenye kazi ingawa kuna vipengele vingine mhusika yeyote anacheza,” anasema Lamata.
“Hayo mambo yanazungumzwa lakini inabidi wakubaliane na hali halisi tu ili kuifanya kazi hii kwenda mbele zaidi.”
Anasema, kutokana na hali hiyo imembidi hata kuwalipia gym wasanii wake ili wafanye mazoezi na kufanya mionekano yao kuvutia.
“Huwezi kumchezesha msichana au mwanamume bonge, tumbo hilo mbele kwenye filamu, hivi nani atakuwa na muda wa kumwangalia lakini akiwa anavutia mambo yanakuwa mazuri,” anasema Lamata.

SOKA NINI, MPANGO MZIMA YEYE NBA, STEVE KERR
Licha ya kuwa shabiki wa Yanga, Lamata anaweka wazi kwake yeye soka si kama mpira wa kikapu na hata ndani kwake ameweka picha ya mchezaji wa mchezo huo, Steve Kerr.
“Napenda zaidi mpira wa kikapu kuliko soka. Soka sifatilii zaidi ya kipindi kile tupo wadogo lakini kikapu naangalia na nafatilia,” anasema Lamata.
“Ndio maana umeona hata hapa nyumbani kwangu unaona picha ya Kerr japo kwa sasa amekuwa kocha anafundisha timu ya Golden State Warriors. Hata hivyo, naendelea kumfuatilia huko alipo kutokana na mapenzi niliyonayo kwake. Alikuwa ni mchezaji mzuri na tishio hasa kwa wale ambao walikuwa wanafuatilia mpira huo kipindi anacheza.
“Nikiwa na nafasi kama si kuangalia kikapu naangalia filamu au kuandika stori kwa ajili ya kazi zangu mwenyewe. Hiki kitu nimekijenga katika akili yangu na huwa hakinipi shida,” anasema Lamata ambaye amepata Tuzo ya Malkia wa Nguvu.

MAZOEZI KWAKE SIO ISHU KUBWA
Ukimwangalia Lamata kimwonekano ni mnene sana, wakati mwingine unaweza kukataa ndio kwanza amefikisha umri wa miaka 30. Pamoja na hilo, hana hata mpango wa kufanya mazoezi ili apungue.
“Nitakuwa mwongo kama nasema huwa nafanya mazoezi, mimi si mfanyaji wa mazoezi kabisa kwa sababu sipendi na sina muda wa kufanya hivyo. Kama nilivyokwambia awali mimi napenda kula, mambo ya msosi hapa ndio penyewe,” anasema Lamata ambaye anapendelea kinywaji aina ya soda, Fanta.

MCHONGO WA KAPUNI
Lamata anafafanua namna alivyopata mchongo wa tamthilia yake hiyo ya Kapuni kurushwa katika televisheni ya DSTV chaneli ya Bongo Magic Movie na sasa ukiwa msimu wa tatu.
“Tulipeleka maombi Watanzania wengi, lakini namshukuru Mungu kazi yangu ilichaguliwa. Nafikiri kuna vitu ambavyo waliviangalia kwangu ni jambo jema,” anasema Lamata na kufafanua mshiko wa kazi hiyo ni makubaliano waliyofanya mwanzo lakini hakuweka wazi thamani.
Ukiingia ndani kwake, kuna sehemu maalumu amehifadhi vitabu vinne vikubwa na ndio kuna mpango mzima wa tamthilia hiyo kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Ni vitabu vinne vyote ni hadithi ya Kapuni kama unavyoona, kuna sini 700, kazi yetu tunaifanya kupitia vitabu hivyo na kuleta kwenye uhalisia kwenye rekodi,” anasema Lamata.
Kupitia tamthilia hiyo amefanikiwa kuajiri watu 82, kati ya hao 61 ni waigizaji na 21 wapo kwenye mitambo yaani wasimamizi, washika kamera na mambo mengine: “Nimetoa ajira tunasaidiana kama unavyoona idadi ya watu hao ni wengi kiasi.”
Anaweka wazi kipengele ambacho anakipenda katika tamthilia hiyo: “Ni pale mtaani ambako Gabo na mkewe wanaishi, mazingira na namna wanavyoishi napenda.”

WASUMBUFU WA KAPUNI         HAWA HAPA
Anasema katika tamthilia hiyo wasanii ambao wanasumbua wanapokuwa wanarekodi ni Romy Jons ‘Jordan’ na  Paul,  jambo ambalo linafanya wapoteze muda mwingi.
“Kama kuna kipengele ambacho Jordan au Paul wanarekodi lazima uwe makini kwa sababu kutokana na ucheshi wao muda mwingi huwa wana kazi ya kuchekesha tu, sasa kama hauko makini mnaweza kutumia muda mwingi kwa sababu ya kurekodi sehemu inayowahusu wao tu,” anasema Lamata.
Akimzungumzia Jordan ambaye ni msanii mpya lakini anafanya vizuri kwenye tasnia hiyo, ndiye alimtengeneza hadi akafikia alipo sasa.