Brazil mabingwa wapya Copa Amerika

Muktasari:

Timu ya Brazil imetwaa Kombe la Amerika, baada ya kuichapa Peru mabao 3-1, katika mchezo wa fainali.

Rio de Janeiro, Brazil. Gabriel Jesus amefunga bao na kutengeza jingine, lakinin aliishia kulimwa kadi nyekundu katika mechi ya fainali ya Kombe la Copa Amerika.

Brazil jana usiku ilitwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 12 kwa kuichapa Peru mabao 3-1.

Mshambuliaji huyo wa Manchester City, alifunga bao la pili dakika ya 45 na dakika 70 alipewa kadi nyekundu.

Wakati akitoka uwanjani Jesus, aliyekuwa akilia alipiga chupa ya maji na kusukuma kifaa cha teknolojia ya uamuzi (VAR).

Matokeo hayo ni makubwa kwa Brazil tangu ilipotwaa dhahabu katika michuano ya Olimpiki mwaka 2016.

Jesus alionekana kurejea katika kiwango  chake kwenye michuano hiyo baada ya kushindwa kung’ara katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka jana ambapo hakufunga bao katika mechi tano alizocheza.