Ushindi waipa matumaini Azam kutetea ubingwa Kagame Cup

Muktasari:

Azam ni mabingwa watetezi wa mashindano ya Kagame baada ya kulitwaa taji hilo mwaka jana

Dar es Salaam. Benchi la ufundi la Azam limedai kuwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mukura FC ya huko Rwanda, utakuwa chachu kwa timu hiyo kutetea ubingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame)

Bao la mshambuliaji mpya wa Azam, Iddi Seleman 'Nado' dakika ya 78 lilitosha kuipa ushindi Azam kwenye mechi yake ya kwanza kwenye mashindano hayo mwaka huu yanayofanyikia huko Rwanda.

Kocha wa Azam FC, Etienne Ndairagije alisema ingawa timu yake ilionyesha kasoro kadhaa kwenye mechi hiyo, ushindi walioupata ni jambo la muhimu zaidi kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

"Nashukuru Mungu kwa sababu tulipata nafasi tukaitumia. Nao walipata lakini bahati haikuwa upande wao. Kikosi changu ni timu ambayo tulikuwa tunaanza kuichanganya wazoefu na vijana tumeweka.

Naona kuwa inaanza vizuri na wameanza kuzoeana. Spidi bado iko chini lakini nina imani kuwa huko mbele tutaendelea kuwa bora zaidi.

Lazima tuendelee kupambana hadi mwisho. Tunajua kuwa hauwezi kuwa bingwa bila kutumia nguvu nyingi. Kwa hiyo tunafahamu hilo ndio maana tukapambana na tukapata ushindi," alisema Ndairagije.

Azam itacheza mechi yake inayofuata dhidi ya KCCA ambao utachezwa mnamo Julai 9 ikishinda itafuzu hatua ya robo fainali.