Kocha Simba aisifu Gor Mahia kumnasa kipa Kisu
Muktasari:
Kisu aliwahi kuichezea Njombe Mji kabla ya Singida United, amejiunga na mabingwa hao wa Kenya kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu, utakaomalizika kipindi kama hiki 2022.
Dar es Salaam.Kocha wa zamani wa Simba na Black Leopards ya Afrika Kusini , Dylan Kerr amesema Gor Mahia ‘K’Ogalo’, limelamba dume kumsajili kipa wa Mtanzania David Kisu kutoka Singida United.
Kerr alisema K’Ogalo wamefanya usajili wa maana kwa kumsajili Kisu ambaye atawaletea changamoto ya namba, Boniface Oluoch, Fredrick Odhiambo na Shaban Odhoji.
Kocha huyo ambaye alimnoa Kisu pindi akiwa Simba alisema, “Ni kipa mzuri ambaye umri wake bado mdogo, anayeweza kuisaidia klabu.”
“Anatabia nzuri, alikuwa akifundishwa na Idd (alipokuwa naye Simba) na kwa sasa atakutana na Willis Ochieng, atakuwa bora zaidi.”
Kerr ambaye aliinoa Gor Mahia na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya (KPL) , 2017 aligomea mkataba mpya na kuamua msimu uliopita kujiunga na Black Leopards.
K’Ogalo wapo katika harakati za kutaka kukiboresha kikosi chao baada ya kuondokewa na mchezaji wao muhimu, Francis Kahata ambaye amejiunga na Simba ya Tanzania na Jacques Tuyisenge aliyetimkia, Petro Atletico ya Angola.
Hata hivyo, imewanasa wachezaji wengine sita wapya mbali na Kisu ambao ni Tobias Otieno, Abdalla Shura, Elvis Ronack, Curtis Wekesa, na Dennis Oalo huku Dickson Ambundo akiwa kwa mkopo akitokea Alliance ya Mwanza.