Nyuma ya Pazia: Frank Lampard tukutane Desemba 25

Muktasari:

Hatimaye Waingereza wameitengeneza ndoto ya Frank Lampard kuwa kocha wa Chelsea. Sijui aliyeamua hivi ni tajiri, Roman Abramovich peke yake au wale wazee  wahifadhina wa Chelsea lakini ndio hivyo, tayari Frank Lampard amekuwa kocha wa Chelsea.

NENO la Kiingereza ninalolipenda zaidi, fairytale. Lakini Waingereza wanalipenda zaidi yangu. Sijaelewa maana yake halisi kwa Kiswahili lakini ni kama vile hadithi tamu. Kama  hii ya Frank Lampard kuwa kocha wa Chelsea.
Waingereza wanakifikirisha kitu, wanakiumba, kinatokea. Walitamani siku moja Frank Lampard au John Terry mmoja wao awe kocha wa Chelsea. Kama walivyotamani siku moja Tony Adams au Patrick Vieira au Thierry Henry, mmojawao awe kocha wa Arsenal. Ni kama walivyotamani siku moja Ryan Giggs au Gary Neville au Roy Keane mmojawao awe kocha wa Manchester United siku za usoni. Wanajaribu kuunganisha mafanikio yako  katika jezi, kisha wanaamini utafanikiwa hivyo hivyo ukiwa katika suti yako maridadi kama kocha.
Hatimaye Waingereza wameitengeneza ndoto ya Frank Lampard kuwa kocha wa Chelsea. Sijui aliyeamua hivi ni tajiri, Roman Abramovich peke yake au wale wazee  wahifadhina wa Chelsea lakini ndio hivyo, tayari Frank Lampard amekuwa kocha wa Chelsea.
Amekuwa kocha kamili kwa msimu mmoja tu akiwa na Derby County. Akaifikisha timu katika hatua ya mtoano kuelekea kupanda Ligi Kuu ya England. Imeonekana kuwa dalili  tosha kwamba akienda Chelsea anaweza kufanya makubwa.
Waliompa timu inawezekana wamefikiria mambo matatu. Kwanza kabisa wamehisi huenda Lampard akawa kocha mzuri baada ya msimu wake wa kwanza tu kama  kocha kuifikisha Derby County mbali.
Hapo hapo wakawaza kama ameifikisha Derby pale basi anaweza kuifikisha Chelsea mbali zaidi kwa sababu atakwenda katika klabu kubwa yenye pesa, huduma nzuri, wachezaji wazuri na bajeti nzuri.
Lakini zaidi ni kwamba Lampard anaijua vema timu. Ni kama nilivyoandika hapo mwanzo wachezaji mahiri wa zamani huwa wanatamaniwa kurudi tena klabuni kwa  sababu wanaelewa miiko na tamaduni za timu. Wanaelewa mashabiki wanataka nini. Wanaelewa mahitaji ya kila kitu katika timu.
Hapa ndipo ambapo mabosi wengi wanaingia mtegoni kuwapa mastaa wa zamani kazi. Wapo wachache waliofanikiwa. Mmoja wapo ni mtu anayeitwa Johan Cruyff.
Nilimuandika wiki iliyopita. Jinsi alivyocheza kwa mafanikio Barcelona. Baadaye akawa kocha klabuni hapo hapo na akapata mafanikio makubwa zaidi. Na wakati kizazi cha zamani kikimkumbuka Cruyff basi kizazi cha sasa kina mtu anayeitwa Pep Guardiola. Huyu ndiye kiini hasa cha mtu kama Lampard kupewa kazi Stamford.
Pep amekuwa akiwatesa mabosi wengi wa soka watafute Pep mpya kupitia mastaa wao wa zamani. Mambo aliyofanya Barcelona yalitamanisha sana. Pep alicheza Barcelona kwa muda mrefu. Alipostaafu akawa kocha wa vijana. Baadaye akaibukia kuwa kocha wa wakubwa kina Lionel Messi, Xavi Hernandez, Andres Iniesta na  wengineo. Mambo aliyofanya Barcelona hauhitaji kusimulia sana. Hii ndio sababu ya kuamini kuwa kuna kizazi cha makocha wa zamani lazima kiondoke halafu kije kizazi cha Pep na katika staili ya Pep.
Kizazi cha mchezaji wa zamani kuibuka kuwa kocha wa timu kubwa miaka michache baada ya kustaafu. Ndicho ambacho Chelsea wamecheza bahati Nasibu kwa Lampard.
Ndiyo, walichofanya ni kamari. Ni bahati nasibu. Wamemtumbukiza Lampard katika kazi ambayo matokeo yake wote hatuna uhakika nayo sana. Hata mashabiki wengi wa  Chelsea hawana uhakika na watakachokipata kutoka kwa Lampard. Walimpenda mno kama mchezaji akiwa ameichezea klabu hiyo mechi 640 na kuibuka kuwa mfungaji bora  wa muda wote na mabao 211 klabuni pale. Lakini hapa Lampard anachukua kazi tofauti na ambayo hana uzoefu nayo.
Kuifundisha Derby msimu mmoja na kuipeleka hatua ya mtoano ya kugombea kupanda daraja ni kitu tofauti na kuipa Chelsea ubingwa wa England mbele ya Pep Guardiola, Mauricio Pochettino na Jurgen Klopp. Hapa ni achilia mbali kwa mtu kama Unai Emery ambaye  anaendelea kujipanga.
Nilimtazama Lampard akiwa na furaha kubwa usoni wakati akitambulishwa mbele ya waandishi wa habari katika uwanja wa mazoezi wa Chelsea Cobham. Sijui kama anakijua  kinachomsubiri lakini Alan Shearer naye alitabasamu vivyohivyo wakati akitambulishwa kama kocha wa Newcastle baada ya kuichezea klabu hiyo kwa mafanikio makubwa.
Kilichofuata ni kwamba Newcastle ilishuka daraja yeye akiwa katika benchi na suti yake maridadi. Thierry Henry hakwenda kuwa kocha wa Arsenal lakini alipojaribu kuwa kocha kamili katika klabu ya Monaco aliishia kuambulia vipigo kila siku mpaka akafukuzwa. Wakati  mwingine ni bora kutoingia hadithi hii au ndoto hii ya kuwa mchezaji mahiri klabuni halafu hapohapo ukajaribu kuwa kocha mahiri.
Kwa Lampard ni wazi kwamba Chelsea imecheza Kamari. Hata hivyo ni mapema kuhukumu. Binafsi nitamchunguza zaidi wakati dunia itakapokuwa inakaribia kuuaga mwaka huu.
Pale Desemba 25 wakati Ligi imechanganya ndio tutajua kama Frank Lampard atahimili ngumi za Ligi Kuu England yenyewe au atakuwa anakaribia kutupa taulo, au atakuwa  ameshatupa taulo na kuinua mikono juu .