Brandy: Naumia nikimwona Shaban Kado benchi

Muktasari:

Tangu waanze kuishi pamoja sasa ni zaidi ya miaka 10, wamefanikiwa kujenga mjengo wa maana huko Kimara, Dar es Salaam, wakiishi na watoto wao wawili, Munira na Fahad.

Dar es Salaam. Nyuma ya mlinda mlango wa Mtibwa Sugar, Shaaban Hassan ‘Kado’ kuna mrembo matata, Brandina Libenanga ‘Brandy Kado’ ambaye anahakikisha kila kitu kinakwenda sawa kwa nyanda huyo aliyeichezea Yanga na Taifa Stars miaka ya nyuma.
Brandy ambaye ni mjasiriamali wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za nyumbani, akifanya biashara kati ya Zanzibar na Dar es Salaam.
Tangu waanze kuishi pamoja sasa ni zaidi ya miaka 10, wamefanikiwa kujenga mjengo wa maana huko Kimara, Dar es Salaam, wakiishi na watoto wao wawili, Munira na Fahad.
Sasa achana na maisha hayo ya nyumbani, Brandy anafichua kinachomuumiza zaidi ni kumwona Kado yako benchi wakati mechi ikiendelea uwanjani.
“Inaniuma na huwa namuuliza kwa nini unakaa benchi, lakini maelezo anayonipa inabidi nimwelewe tu sina namna,” anasema Brandy anayefafanua kuwa, Kado ni mpenzi wa ndizi nyama na chapati za maji.

ANAVYOWAPOTEZEA
Kama unavyojua, si kitu kigeni kwa baadhi ya wanawake kuwashobokea wachezaji. Inaweza kuwa kwa sababu ya mapenzi ya soka tu, lakini wakati mwingine huwatamani kimapenzi.
“Vinaniumiza na sipenzi lakini kama mwanamke najua namna gani niweze kuifanya familia yangu kuwa na amani. Unaweza kwenda kwenye mpira unaona mashabiki wanavyomshangilia wengine wanamfuata kumpongeza, kupiga naye picha na kumposti kwenye mitandao ya kijamii,” anasema Brandy.
“Binafsi huwa ni mwelewa kwani kuna marafiki zake hata kama ni wanawake, ingawa wakati mwingine wapo wanaomnyemelea. Kama nimekubali kuwa mke wa mchezaji ambaye ni staa, natakiwa kuishi hivyo na nimejitengeneza kisaikolojia.”

HII KADO HAPENDI KABISA
Mwanamke huyo mwenyeji wa Morogoro anasema:
“Kado hapendi kabisa niwe na makundi au kutangatanga, anapenda nitulie nyumbani na kufanya mambo ya muhimu kwa ajili ya familia.
“Anataka ujiheshimu kama mke wa fulani, lakini si kuwa na tabia ambazo ukitembea kila mtu anakuguna.”

KADO KUMBE YUKO HIVI
“Kusema kweli najivunia kuwa na Kado, nimepata mwanaume mpole hana gubu na upendo kwa familia.  Nyumba yetu ina furaha na amani kwa kweli jambo linalonifanya hata anapokosekana nyumbani nimmisi zaidi,” anasema Kado.
“Hata anapokuwa kwenye mapumziko kama hawana majukumu kwenye timu, Kado anakuwa mtu wa nyumbani kuzungumza na familia na akitoka anakwenda gym kwa ajili ya mazoezi.