Kaa chonjo Simba mpya inashambulia muda wote

Muktasari:

Kutokana na aina ya wachezaji iliowasajili na wale waliopo kikosini, benchi la ufundi la Simba lina uwanda mpana wa kuchagua aina yoyote ya mfumo ambao itautumia katika mpango huo wa kushambulia kutegemea na mechi husika na ubora wa wapinzani wao.

MASTAA tisa (9) wametua kwenye kikosi cha Simba kwenye dirisha hili la usajili ambao wanategemewa kuungana na wengine waliobakia kuunda kikosi cha timu hiyo msimu ujao ambapo watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu, Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi.
Aina ya usajili ambao Simba imefanya, inatoa picha ya wazi kuwa akili na mipango ya benchi la ufundi la Simba ni kusaka zaidi mabao msimu ujao kwani kundi kubwa la nyota waliotua na hata wale waliobakizwa wamekuwa na hulka ya kupenda kushambulia.
Kwanza kuna beki kiraka wa kati Gerson Fraga Vieira, raia wa Brazil, ambaye ana uwezo mkubwa wa kukaba na kuilinda timu lakini pia anajua kuchezesha timu, kupiga pasi za mwisho na hata kufunga mabao pindi anapopata nafasi ya kufanya hivyo.
Sifa hizo pia zinaenda na zile za Mbrazil mwenzake Tairone Santos Da Silva ambaye naye anacheza nafasi ya beki wa kati, lakini imemnasa kiungo mshambuliaji anayejua kupiga pasi za mwisho, Sharaf Shiboub kutoka Sudan. Pia, wamo winga mwenye uzoefu Deo Kanda kutoka DR Congo, Miraji Athuman Kutoka Lipuli, mshambuliaji Wilker Henrique da Silva, beki Kennedy Juma na kiungo mshambuliaji aliyekuwa Yanga, Ibrahim Ajibu, beki Gadiel Michael na kiungo Francis Kahata kutoka Kenya bila kumsahau kipa Beno Kakolanya.
Kutokana na aina ya wachezaji iliowasajili na wale waliopo kikosini, benchi la ufundi la Simba lina uwanda mpana wa kuchagua aina yoyote ya mfumo ambao itautumia katika mpango huo wa kushambulia kutegemea na mechi husika na ubora wa wapinzani wao.

4-2-3-1
Katika mfumo huu, ambao unalenga kuwabana wapinzani kuanzia kwenye eneo lao la ulinzi, Simba inaweza kuanza na kipa Kakolanya ama Aishi Manula, beki wa kulia akacheza Shomary Kapombe na kushoto akacheza Mohammed Hussein kwa vile hauhitaji sana mabeki wa pembeni kupanda.
Mabeki wa kati wanaweza kuanza Erasto Nyoni na Wawa wakati viungo wawili wa chini wakacheza Jonas Mkude na Gerson Vieira, mbele yao kukawa na Chama, Shiboub na Kahata huku mbele akisimama Kagere.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Crecentius Magori alisema kuwa jukumu la uongozi ni kutimiza mahitaji ya kocha na baada ya hapo kazi itabakia kwa benchi la ufundi.
“Kikosi kinachosajiliwa ni kizuri kwa sababu kimetokana na mapendekezo yake yeye mwenyewe kocha na ndiye mwenye jukumu la kujua nani acheze na nani asicheze,” alisema Magori.
Lakini kwa viungo watatu wanaocheza mbele ya wale wawili wa chini, Simba inaweza kuwatumia Ajibu, Chama na Deo Kanda huku mbele akianza Bocco.

4-4-2
Ni mfumo ambao kocha Patrick Aussems amekuwa akipendelea kuutumia na si ajabu ndio maana amependekeza kusajiliwa kwa mawinga Deo Kanda na Miraji Athuman.
Hapa kikosi kinaweza kuwa hivi Manula/Kakolanya, Kapombe, Gadiel/Tshabalala, Vieira, Nyoni, Mkude, Kanda, Shiboub, Bocco, Kagere, Chama ama kinaweza kuwa hivi, Kakolanya/Manula, Kapombe, Tshablala/Gadiel, Wawa, Tairone Santos, Nyoni, Kahata, Chama, Wilker Da Silva, Ajibu, Miraji Athuman.

3-5-2
Mfumo huu unahitaji mabeki wawili wa pembeni ambao wanaweza kucheza kama mawinga na wakatimiza jukumu la ulinzi wakati huohuo sambamba na viungo asilia watatu hivyo ni wazi kwamba Gadiel Michael na Kapombe wataanza kama mabeki wa pembeni.
Lakini kunatakiwa kuwepo na mabeki watatu wa kati ambao wana utulivu na umakini wa hali ya juu pamoja na uwezo wa kuchezesha timu kuanzia nyuma na angalau mmoja awe anatumia vyema mguu wa kushoto hivyo kikosi kinaweza kuwa hivi Manula/Kakolanya, Kapombe, Gadiel, Vieira, Wawa, Nyoni, Mkude, Chama, Mzamiru/Kahata, Kagere, Bocco/Wilker da Silva.

4-3-3
Kutokana na Kanda kuwa na uwezo wa kufunga mabao kama ilivyo kwa Chama na Ajibu, kwenye mfumo huu wanaweza kutumika kama washambuliaji wa pembeni.
Hata hivyo, Ajibu na Chama wanaweza pia kuchezeshwa kama kiungo anayecheza nyuma ya mshambuliaji.
Manula/Kakolanya, Kapombe, Gadiel/Tshabalala, Wawa/Tairone, Nyoni/Vieira, Mkude/Mzamiru, Kahata/Hassan Dilunga/Shiboub, Kanda/Ajibu, Kagere/Bocco/Wilker da Silva na Chama/Miraji.

3-4-3
Kwenye mfumo huu watatu kati ya Tairone, Vieira, Nyoni au Wawa wanaweza kuanza kama mabeki wa kati na mbele yao kukawa na Kapombe, Gadiel, Mkude na Shiboub, washambuliaji watatu wakaanza Kagere, Bocco na Wilker Silva au wengine watatu wa mbele wakacheza Ajibu, Chama na Deo Kanda. Hata hivyo, bado kuna kundi lingine la wachezaji ambao wanaweza kupata nafasi kikosini ambao ni Kennedy Juma, Mohammed Ibrahim, Said Ndemla, Rashid Juma, Ally Salim na Mohammed Rashid.