MAJANGA! Marcelo ashindwa kufanya mazoezi leo, Stars ikijiandaa kuivaa Senegal

Monday July 1 2019

Majanga Kenya, Marcelo ashindwa, kufanya mazoezi leo, Stars ikijiandaa kuivaa Senegal, Mwanasport, Mwanaspoti

 

By Fadhili Athumani

Cairo, Misri. Muda mfupi kabla ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, kujitosa uwanjani, kucheza mechi yake ya mwisho ya Kundi C, dhidi ya Simba la milima ya Teranga, hofu imetanda kikosini kuhusu hali ya beki wake wa kushoto, Eric Ouma ‘Marcelo’, baada ya jana jioni, kushindwa kufanya mazoezi na timu.

Awali ilidhaniwa kuwa Marcelo, ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa Tanzania, katika mchezo wa pili ambao Kenya ilishinda 3-2, angekuwa sawa lakini kwa mujibu wa timu ya madaktari wa Stars, kuna kila dalili kuwa, Ouma atakosa mchezo wa leo, ambao ni muhimu kwa timu zote mbili.

Kenya na Senegal zitajitosa uwanjani, katika dimba la Jeshi, Jijini Cairo, kuanzia saa nne usiku, kuwania nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora ya fainali za mataifa ya Afrika, zinazoendelea kutimua vumbi, huku zote zikihitaji ushindi.

Kenya iliyo katika nafasi ya tatu na Senegal, iliyo katika nafasi ya pili, zote zina alama tatu, huku zikizidiana kwa tofauti ya mabao. Kama ni kweli Ouma amepata jeraha, atakuwa mchezaji wa tatu, kujeruhiwa mazoezini muda mfupi kabla ya mechi kubwa.

Taarifa hizi ni mbaya sana kwa Kenya, ambayo inatarajia kufuzu hatua inayofuata ya makala haya ya 32. Hata hivyo, afueni ni kwamba, beki wa kati Joash ‘Berlin Wall’ Onyango, aliyekosa mechi ya Algeria na Tanzania anarejea kikosini leo jioni kuivaa Senegal.

Beki mwengine aliyerejea kikosini na kuongeza morali ya timu ni beki wa kulia wa Gor Mahia, Philemon Otieno, ambaye yeye alilazimika kukaa nje katika mchezo wa Stars dhidi ya Tanzania.

Advertisement

Bundi huyu wa majeruhi, ameendelea kuinyanyasa Kenya, ambapo itakumbukwa pia kuwa, mbali na Joash, Ouma na Otieno, pia aliwatembelea beki wa kati, Musa Mohammed, ambaye hata hivyo alipona haraka na kuwahi mechi ya kwanza na mwenake Brian Mandela.

Advertisement